Jana Gazeti la Mwananchi lilichapisha habari ya mwanafunzi huyo ambayo pia leo iliwekwa kwenye mitandao yake ya kijamii ikieleza namna mwanafunzi huyo anavyohangaika kulipa deni hilo ili apatiwe kitambulisho chake cha Nida.
Saa chache baadaye, Waziri Ummy aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram akiambatanisha na picha ya Lightness, akiagiza mwanafunzi huyo afike Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila akachukue kitambulisho chake.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajali wananchi wake. Mwenye mawasiliano na huyu binti anipatie inbox. Kesho saa 4 asubuhi afike Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila akachukue kitambulisho chake, Akamuone Mkurugenzi wa Hospitali ya Mloganzila.
Wakati Sera ya Afya ya mwaka 2007 inataka wananchi kuchangia huduma za Afya, bado Serikali inatambua kuwa wapo wananchi wengi ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu hususani katika kipindi hiki cha maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo matibabu yana gharama kubwa.
Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali inakuja na Sheria ya Bima ya Afya kwa kila mtu (Universal Health Insurance) ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila ya kikwazo cha fedha.” ameandika Waziri Ummy nakuongeza
“Ni matumaini yetu kuwa tukiwa na utaratibu huu wa Bima ya Afya kwa kila mtu (wananchi wengi wazima watachangiana kidogo kulipia wananchi wachache watakaokuwa wagonjwa tofauti na sasa ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wanaojiunga na Bima kwa hiyari ni wagonjwa) masuala haya tutayapunguza kama sio kuyamaliza kabisa.
Pia, narudia tena kuzitaka Hospitali zote za Serikali nchini kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya kuwa “kila baada ya siku chache kuprint bill ya mgonjwa (Ankara ya mteja) ili ndugu waweze kulipia na hii itasaidia kuwapunguzia mzigo wa kulipa ankara kubwa za matibabu kwa mgonjwa wao.”
Lightness ambaye anasoma mwaka wa pili katika chuoni cha LGTI, alisema hivi karibuni kuwa baba yake, Priscus Shirima alifariki Julai 4, mwaka huu katika hospitali hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kulazwa kwa siku 40 na kuacha deni.
Ili kuwa na uhakika deni hilo litalipwa, uongozi wa hospitali hiyo unadaiwa kumtaka mwanafunzi huyo kutoa kitambulisho cha Nida kama dhamana na kupewa mwili wa baba yake kwa sharti la kulipa Sh50,000 kila mwezi.
Lightness aliiambia Mwananchi kuwa baba yao aliugua shinikizo la damu ambalo lilimpelekea kupofuka macho na kupata kiharusi.
Alisema anapaswa kulipa deni la baba yake katika hospitali hiyo licha ya kwamba bado ni mwanafunzi na kuiomba Serikali impe msamaha wa deni hilo kwa kuwa hana uwezo wa kulilipa.
Alisema baada ya baba yake kufariki, familia walitaka kuchukua mwili na kwenda kuuzika nyumbani kwao Rombo, mkoani Kilimanjaro, hata hivyo walikuta deni la Sh9 milioni ambalo hawakuwa na uwezo kulilipa.
Lightness alisema uongozi wa hospitali ulimtaka atoe kitambulisho chake cha Nida ikiwa ni dhamana ya kukomboa mwili wa baba yake ukazikwe.
Uongozi wa hospitali hiyo ulikiri kuidai familia hiyo Sh9 milioni gharama za matibabu ya mgonjwa kukaa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa siku 40 mfululizo.