MICHAEL Mrema, mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema, ameeleza walichoteta na baba yake kabla ya umauti kumfika juzi.
MICHAEL Mrema, mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema.
Akizungumza nyumbani kwa baba yake jana mkoani Dar es Salaam, Michael alisema kuwa Jumamosi ya Agosti 20 saa 11 jioni walipata nafasi ya kuzungumza na baba yake na miongoni mwa alichowaambia ni kuishi kwa upendo, amani na kupendana katika familia yao.
“Siku ile ya Jumamosi (Agosti 20) tulipozungumza naye akiwa yuko vizuri na anacheka tu, hatukutegemea kama Jumapili asubuhi angetuacha.
"Baada ya kuzungumza naye, tulifanya maombi kumwombea apone haraka na miongoni mwa alichozungumza ni kututaka tuishi kwa amani, kupendana na kuishi salama kama familia,” alisema Michael.
Alisema miongoni mwa vitu ambavyo hawatovisahau kwa baba yao ni ucheshi.
“Baba amefanya mambo makubwa ikiwamo kutusomesha na tukapata kazi nzuri. Kama unavyoona hapa ndio kwake, lakini sisi watoto wake tumejenga tumemzunguka, wote tunaishi sehemu moja, kwa hiyo ukitaka kutoka barabarani ilikuwa ni lazima tupitie kumwona.
“Miongoni mwa vitu tutakavyomkumbuka ni ucheshi wake, kwa sababu tulikuwa karibu naye, ilikuwa rahisi kuja kuleta hata wajukuu hapa kuongea naye, alikuwa ni rafiki yetu,” alisema.
Msemaji wa Familia hiyo, Alex Mrema, alisema kaka yake alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Agosti 15 mwaka huu alikokuwa akipatiwa matibabu na kufariki dunia Agosti 21.
Alisema kaka yake atazikwa keshokutwa katika Kijiji cha Kiraracha, Marangu Magharibi mkoani Kilimanjaro na kabla ya hapo, kesho mwili wake utaagwa nyumbani kwake Salasala, Kinondoni saa tano asubuhi na kisha kufanyiwa ibada katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Augustino saa saba mchana.
"Taratibu za maziko zinaendelea vyema. Kabla ya maziko yake, atapelekwa katika Kanisa la Bikira Maria, Malkia wa Rozari Takatifu Uomboni kwa ajili ya ibada ya maziko.
"Hivi sasa kuna vikao vingine vinaendelea Dar es Salaam na leo jioni (jana), tutafanya kikao hapa nyumbani kwake Kiraracha," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, alisema msibani jana kuwa watamkumbuka Mrema kama mpenda amani na mhamasishaji wa maendeleo kwa mkoa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, alisema wanaoingia kwenye siasa wanapaswa kujifunza kutoka kwa Mrema.
*Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Sabina Ntobi (TUDARCo) na Mary Mosha (MOSHI)