Yanga Yanukia CAF Super League


MASHABIKI wa Yanga waliingiwa na ubaridi baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba watani zao, Simba ndio timu pekee itakayoshiriki michuano mipya ya CAF Super League, lakini kwa sasa hawapaswi kuwa na presha kwani, huenda timu yao ikashiriki kama mipango itaenda inavyopangwa na Cecafa.

Tangu michuano hiyo ilipozinduliwa juzi jijini Arusha kwenye Mkutano wa CAF, Yanga walikuwa wanyonge kwa kutambiwa na wenzao kwamba wao ni wazee wa hapahapa kwani Simba itashiriki, lakini Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Rais wa Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Wallace Karia amefichua timu shiriki bado hazijafahamika.

Karia alisema CAF imezipa Cecafa na Cosafa (Baraza la Soka Kusini mwa Afrika) nafasi 12 kutokana na vigezo mbalimbali na Tanzania huenda ikawa na zaidi ya timu moja na hazizidi tatu na kwa rekodi zao katika michuano ya Cecafa, Simba, Yanga na Azam zote zina nafasi ya ushiriki.

“Tanzania inaweza kuwa timu zaidi ya moja kwenye michuano hiyo kulingana na vigezo vilivyowekwa kwani Cacefa na Cosafa zimepewa nafasi 12, hivyo zitaibeba timu zetu, imani yangu hazitazidi tatu wala kupungua chini ya moja,” alisema Karia.

Karia alisema kwa Mkutano Mkuu wa CAF kufanyika Tanzania ni historia kubwa kwa nchini na kuitangaza duniani na hasa ushiriki wa Rais wa Shirikisho la Kimataifa (FIFA) Gianni Infantino ambaye ilikuwa mara ya pili kwake kuzuru nchini.

Michuano hiyo ya Super League imepangwa kufanyika mwakani kati ya Agosti 23 hadi Mei 2024 ikishirikisha klabu 24. Klabu shiriki kila moja itapata Dola 2.5 milioni zaidi ya Sh 5.8 bilioni na bingwa wake atazoa Dola 11.5 milioni ni kama Sh 27bilioni, huku michuano hiyo ikiwa na thamani ya Dola 100milioni (Zaidi ya Sh233 bilioni).

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, juzi alinukuliwa alisema michuano hiyo itaongeza thamani ya soka la Afrika, japo hakufafanua kama timu hiyo itashiriki, japokuwa alisisitiza anaona nafasi kubwa ya kuzisaidia klabu kiuchumi na kukuza soka la Afrika.

“Tofauti ni uwekezaji, ukiangalia Michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho hauwezi kufananisha na Ligi ya Mabingwa Ulaya ama Europe League, hii CAF Super League tunaona kama jambo kubwa na mwishowe soka ni hela pia uwekezaji bila ya hilo hatuwezi kufanya vizuri,” alisema Barbara.

Simba na Yanga zitaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Geita Gold na Azam zitacheza Kombe la Shirikisho, Wanalambalamba wataanzia raundi ya pili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad