Zimwi la ajali lazidi kutafuna watu nchini




Singida/Dodoma. Zimwi la ajali limeendelea kugubika katika maeneo mbalimbali nchini na kupoteza maisha ya watu, huku wengi wakiachwa kwenye ulemavu na uharibifu wa vyombo vya usafiri.

Juzi jioni, watu watano walipoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa baada ya basi la Tanzanite kupinduka katika Kijiji cha Mbwasa, wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Ajali hiyo ilitokea wakati basi hilo aina ya Higer lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam lilipopinduka zikiwa zimepita siku nne tangu kutokea ajali iliyochukua maisha ya watu 19 mkoani Mbeya na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wamependa kuligonga kwa nyuma lori la mizigo.

Ajali hizo ni mwendelezo wa ajali ambazo zimetokea siku za hivi karibuni katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Simiyu, Arusha, Shinyanga na kusababisha vifo na majeruhi.


Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk Ernest Ibenzi jana alithibitisha kupokea majeruhi kadhaa kutoka katika ajali hiyo na kwamba wengi walitibiwa na kuruhusiwa, lakini wanne kati yao walikuwa wanaendelea na matibabu.

“Tulipokea mwili mmoja na majeruhi kadhaa, lakini tuliwaruhusu karibu 14 na mmoja alikuwa ameumia kichwani; tulimpeleka Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa matibabu zaidi, wanne tunaendelea nao hapa na hali zao zinazidi kuimarika,” alisema Dk Ibenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi mchana wakati basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Abdul Kingwande lilipopinduka wakati likishuka kwenye Mlima Saranda.


Kamanda huyo alisema majeruhi 15 walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General Dodoma), kwa ajili ya matibabu na baada ya uchunguzi na kupata matibabu, abiria 10 waliruhusiwa.

Aliwataja waliopoteza maisha ni Diwani wa Iramba, Mwinjuka Mkumbo (40) aliyefia hospitali wakati akipatiwa matibabu, mtoto Alicia Flagence (01) na wengine watatu ambao miili yao haijatambuliwa hadi jana jioni.

“Hadi sasa majeruhi Sharifati Mwipi (32), Rudia Daniel maarufu Kudia (59), Saidi Mbwana (39) na Adul Ramadhan (32) wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na hali zao zinaendelea kuimarika,” alisema Mutabihirwa.

Hata hivyo, alisema majeruhi mwingine, Ngisa Sita (26), alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na hali yake kuhitaji madaktari bingwa.


Kuhusu dereva wa basi hilo, Abdul, Kamanda huyo alisema alitoroka baada ya kutokea kwa ajali na polisi wanaendelea kumsaka ili kumfikisha katika vyombo vya sheria.

Akizungumzia chanzo cha ajali, alisema uchunguzi wa awali umebaini mwendokasi wa dereva wa basi hilo ndio ulisababisha ashindwe kulimudu baada ya kupoteza mwelekeo na kuacha njia kisha kupinduka.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Enoset Msangi alisema kifo cha diwani wao kimewastua wengi kwa sababu alikuwa tegemeo la watu katika halmashauri hiyo.

Msangi alisema mwili wa diwani huyo aliyekuwa wa viti maalumu, utazikwa Jumapili mchana baada ya taratibu zote kukamilika.


Ajali ya Mbeya

Agosti 16 mwaka huu watu 19 walipoteza maisha papohapo na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la Shamwengo, karibu na kituo cha mafuta Inyala mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei, tukio hilo lililohusisha gari la Kampuni ya Evarest Frech Ltd, likiwa na kontena la mchanga lilifeli breki na kuligonga basi la Super Rojas lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Njombe.

Alisema baada ya kugonga basi hilo, liliendelea kushuka zaidi na kuligonga gari jingine aina ya Mercedes-Benz na kusababisha vifo vya watu wanane na majeruhi kadhaa waliopelekwa hospitali.

Kamanda huyo alisema miongoni mwa sababu za ajali hiyo ni ufinyu wa barabara na ili kudhibiti matukio ya ajali wameanzisha ukaguzi wa malori yanayotumia njia hiyo.

Shuhuda wa ajali hiyo, Marekani Mwaharemba alisema kabla ya ajali alikuwa kwenye bajaji, aliposhuka dereva wa bajaji hilo alitaka kuingia barabarani, alimkataza akimwambia asiingie kuna hatari.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad