Aeleza kortini ofisa usalama alivyouawa, kuporwa mil. 400/-






MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa jinsi watu wawili wanaodaiwa majambazi walivyomshambulia kwa risasi na kumuua Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Silvanus Mzeru mwaka 2014 maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Watuhumiwa wa mauaji hayo ni madereva bodaboda; Kelvin Lilai na Revocatus Rugalabamu wanaodaiwa kushiriki matukio mawili ya kumpora fedha Mzeru zinazokadiriwa kuwa ni Sh. milioni 400.

Akitoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa hao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde, Sajenti Mohamed (47), alidai watuhumiwa hao pia walimuua mlinzi wa KK Security, Frank Silayo maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Mohamed ambaye ni kiongozi katika kikosi maalum cha upelelezi wa makosa ya mauaji na makosa ya kutumia silaha, alidai kuwa Julai 15, 2014, yeye pamoja na wenzake walipewa maelezo na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillus Wambura kuchunguza mauji ya Mzeru yaliyotokea Aprili 29, mwaka huo.

Alidai baada ya taarifa hiyo, Julai 16, 2014 alikwenda Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kukutana na askari Nicolaus aliyekuwa mpelelezi wa tukio lililotokea uwanja wa ndege, ambapo wakati huo kulikuwa na mtuhumiwa Mohamed Kazembe.

"Nilifanya naye mahojiano na kunieleza yeye ni mhalifu wa matukio ya kutumia silaha, akishirikiana na wenzake Lilai, Chinga, Mashaka Mwafongo, Rugalabamu na Omary Said," alidai shahidi huyo.

Sajenti Mohamed alidai miongoni mwa matukio waliyoyafanya ni la Februari 21, 2014 majira ya saa 3:30 usiku eneo la Oysterbay, walivunja vioo cha gari aina ya Nissan Patrol na kuchukua fedha zinazokadiriwa kuwa ni Sh. milioni 100, mali ya Mzeru.

Alidai kuwa baada ya tukio hilo, wakati wanaondoka kulikuwa na mlinzi wa KK Security ambaye alijaribu kuwafuata na walimfyatulia risasi na kusababisha kifo chake na pia walifanya tukio la pili Aprili 29, 2014 maeneo ya uwanja huo wa ndege.

Alidai katika tukio hilo walifanikiwa kupora fedha za kitanzania na za kigeni zinazokadiliwa kuwa ni Sh. milioni 300 na kusababisha kifo cha Mzeru baada ya kumshambulia kwa risasi na kufanikiwa kumpora fedha hizo.

Sajenti Mohamed alidai walianza kuzifanyia kazi taarifa hizo, ambapo Julai 17, 2014 walipata taarifa kutoka kwa msiri Said kuwa ni dereva bodaboda na kijiwe chake na kuegesha TAZARA, Dar es Salaam.

"Tulishirikiana na msiri tukaweka mtego Julai 18, 2014 saa moja na nusu asubuhi, Said wakati anatoka nyumbani kwake tulifanikiwa kumkamata na tukafanya naye mahojiano," alidai.

Katika mahojiano hayo, Said alikiri kuhusika na matukio hayo mawili ya kumpora Mzeru na pia alishirikiana na Kazembe, Chinga, Mashaka, Rugalabamu, Lilai ambapo aliwaunganisha na kufanikiwa kumkamata Lilai.

Alidai mshtakiwa alikamatwa Julai 19, 2014 eneo la Nangurukuru wakati wakielekea Masasi kumkamata Lilai huku wakielekezwa na mtuhumiwa Said, ambapo kazi yao ilishia hapo baada ya kukutana na mtuhumiwa eneo hilo akiwa na gari lake aina ya IST.

Mtuhumiwa Lilai aliwataja washirika wake na aliwasaidia kumpata mtuhumiwa Rugalabamu, ambapo aliweka mtego na kumkamata Julai 20, 2014 wakafanya naye mahojiano na yeye aliwasaidia polisi kumpata Mwafongo.

Alidai Mwafongo alikiri anamiliki silaha tatu kinyume cha sheria na yeye pamoja na Chinga ndiyo walifyatua risasi katika matukio hayo mawili na silaha zake huwa anazihifadhi kwa dada yake, Lucy Mwafongo anayeishi maeneo ya Vingunguti, Mtaa wa Tupendane.

Alidai walizingira nyumba ya Lucy wakafanikiwa kumkamata na pia walifanikiwa kupata silaha na risasi zilizotajwa na kaka yake, baada ya tukio kuisha walimrudisha Kituo cha Polisi Oysterbay.

Alidai ilipofika saa nane usiku, Mwafongo aliwaeleza polisi kwamba kuna silaha nyingine ameifukia nyuma ya viwanda vya Tanganyika Packers na baada ya kufika eneo hilo mshtakiwa alijaribu kutoroka ndipo akapigwa risasi ya paja na wakati anadondoka risasi nyingine ikampata mgongoni, walimkimbiza hospitalini lakini baadaye walipata taarifa kuwa alipoteza maisha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad