Arusha. Upande wa Jamhuri unatarajia kuwa na mashahidi 14 na vielelezo 17 katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake watatu.
Mbali na Dk Pima washtakiwa wengine ni aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha na uchumi, Mariam Mshana, aliyekuwa mkuu wa idara ya mipango na uchumi, Innocent Maduhu na Alex Daniel.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa leo Septemba 16, 2022 Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Kabla ya kusomea maelezo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule aliomba kubadili hati ya mashtaka na kufanya hati hiyo kuwa na mashtaka sita badala ya manne ya awali.
Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, Wakili Janeth aliieleza mahakama kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi 14 na vielelezo 17, katika kesi hiyo.
"Kwa upande wa jamhuri tunaomba tusiwataje mashahidi wala vielelezo labda kwa idadi, tunatarajia kuwa na mashahidi 14 na vielelezo 17,"amesema
Akiwasomea makosa hayo, Sekule amedai kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu ambapo kati ya Aprili 14 hadi 16,mwaka huu wakiwa waajiriwa wa Serikali kwa pamoja na kwa nia ovu walifanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kwa matumizi yao binafsi Sh65 milioni iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya matumizi ya umma.
Ametaja shitaka la pili ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri kinyume na sheria ambapo wanadaiwa Aprili 14,2022 walimdanganya mwajiri kupitia nyaraka yenye dokezo lililokuwa linahusiana na shughuli za kila siku za mwajiri ambapo walidanganya Daniel amenunua na kusambaza moramu yenye thamani ya Sh65 milioni huku wakijua kwa kufanya hivyo ni kumdanganywa mwajiri.
Alidai shitaka la tatu ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri ambapo, Aprili 14, 2022 wakiwa na nia ovu walitumia nyaraka ya maombi ya masurufu, ikiwa na maelezo ya uongo yakionyesha Daniel amesambaza moramu kwa ajili ya matengenezo ya barabara na anadai Sh65 milioni huku wakijua wanamdanganya mwajiri wao.
Shitaka la nne ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri ambapo wanadaiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu kupitia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari marejesho ya masurufu iliyoandikwa Aprili 26, 2022 iliyohusiana na shughuli za mwajiri.
Alidai nyaraka hiyo ilikuwa na maelezo ya udanganyifu kuwa Alex anafanya marejesho ya Sh65 milioni ikiwa ni matumizi ya kusambaza moramu katika taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kutengeneza barabara huku wakijua kwa kufanya hivyo wanamdanganya mwajiri.
Wakili Janeth ametaja kosa la tano ni kughushi sahihi ambapo alidai kuwa watuhumiwa hao Aprili 28,2022 walighushi sahihi ya Noel Letara ikionyesha amesambaza vifusi kwenye baadhi ya barabara za jamii na maeneo ya taasisi za Serikali.
Amesema kosa la sita linalowakabili wote ni kughushi sahihi ambapo amedai kuwa watuhumiwa hao Aprili 28,2022 walighushi sahihi ya James Raphael, ikionyesha amesambaza vifusi kwenye baadhi ya barabara za jamii na maeneo ya taasisi za serikali.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 28,2022 kwa ajili kutajwa na kuanza kusikilizwa Oktoba 6, 2022.