Kunapokuwa na hali ya hewa ya baridi katika maeneo mengi nchini, mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, huwa ni kwa baadhi ya watu kukataa kuoga wakihofia baridi hiyo, jambo ambalo hufanya watafsiriwe kuwa wachafu.
Kwa maeneo yenye joto, kupitisha siku moja bila kuoga, kunaweza kufanya mtu atafsiriwe kama mchafu na endapo akikaa kwa siku kadhaa, hata harufu ya mwili wake hubadilika. Hebu jiulize mwenyewe, ni kipindi kipi kirefu ambacho umewahi kukaa bila kuoga? Siku moja? Mbili? Wiki? Au wiki kadhaa kipindi ukiwa unaumwa?
Sasa sikia hii, Amou Haji, mwanaume mwenye umri wa miaka 87 anayeishi jangwani nchini Iran ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia kuwa mtu mchafu zaidi, akiwa amekaa kwa takribani miaka 67.
Kwa madai yake, bwana Amou ni kwamba anaogopa maji na hii ndiyo sababu hajaoga kwa zaidi ya miongo sita. Amou anadai kwamba ataugua ikiwa ataoga na ndiyo maana aliamua kutooga kwa zaidi ya miaka 65.
Taarifa zilizoripotiwa na Gazeti la Bongo Times, zinaeleza kuwa Amou anaishi peke yake katika jangwa la Irani lakini hataki kuishi peke yake, anataka kuwa na mwenza. Amou hana nyumba anaishi kwenye mashimo yaliyotengenezwa jangwani nje kidogo ya kijiji.
Chakula anachopenda Amou ni nyama ya nungunungu. Amou hapendi chakula kilichopikwa nyumbani anapenda sana vyakula visivyo jamii ya mboga. Pia anapenda sana kuvuta sigara na anapomaliza sigara anazopewa na wanakijiji, basi huvuta kinyesi kikavu cha wanyama badala ya tumbaku.
Inaelezwa kuwa Amou anapitia hayo baada ya kupata matatizo ya kisaikolojia, yaliyosababishwa na matatizo ya kihisia aliyowahi kukutana nayo katika ujana wake, hali iliyosababisha aamue kuishi maisha ya kujitenga.
Anajiangalia kwenye vioo ila ni vile vioo vya pembeni vya magari yapitayo. Anakunywa lita tano za maji kila siku kutoka kwa kopo kubwa lenye kutu. Anapunguza nywele zake kwa kuzichoma juu na moto.