Anayeidai hospitali fidia mil. 500/- aanza kutoa ushahidi mahakamani



MFANYAKAZI wa Wizara ya Kilimo, Florence Samwel, amedai mahakamani kuwa uchunguzi wa sampuli za tezi aliofanyiwa na Hospitali ya TMJ haukuzingatia weledi.

Pia amesema kulikuwa na uzembe kwa kupewa majibu yasiyo sahihi kuwa ana saratani.

Akitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemalira, alidai uchunguzi uliyofanywa TMJ ulikuwa na majibu tofauti na yaliyotolewa Hospitali ya Apollo kuhusu sampuli hizo yakionesha hana ugonjwa wa Rapillary Carcinoma of Thyroid, kama ilivyodaiwa na Hospitali ya TMJ.

Florence alidai hayo jana wakati akihojiwa na Wakili wa TMJ, Josephat Mabula, katika shauri la madai alilofungua dhidi ya hospitali hiyo, Hindu Mandal na Dk. Moirice Mavura, analodai fidia ya Sh. milioni 500.

Pia alidai sampuli zilizopimwa TMJ ndiyo zilizopimwa na Hospitali ya Apollo, kwa kuwa daktari aliyempa sampuli hizo alimtaka asizifungue na alifanya hivyo.


Kuhusu kiwango cha sampuli 15 zilizopimwa na Hospitali ya Apollo katika ripoti yake ya Januari 31, 2019, Florence alidai hajui jumla ya sampuli hizo kwa kuwa daktari aliyempa alimwelekeza asizifungue.

Florence alidai, hakubaliani na wakili huyo kuwa Hospitali ya Apollo ilitakiwa ijiridhishe kutokana na uchunguzi wake alioufanya na kwamba ana uhakika kuwa daktari wa TMJ hakuwa na weledi katika kazi yake.

Akiendelea kujibu maswali ya wakili huyo, Florence alidai kuwa upasuaji wa tezi aliyofanyiwa na Dk. Mavura, Julai 9, 2018 ulikuwa kimakosa, hakustahili kufanyiwa na pia katika ripoti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ilieleza upasuaji huo ulikuwa ni hatarishi kwake.


Shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 5, 2022 saa sita mchana kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Katika madai yake, Florence alisema Juni 27, 2018 alienda Hospitali ya Muhimbili na kufanyiwa uchunguzi wa koo ambako alielezwa amuone Dk. Mavura.

Alidai, baada ya kumwona Dk. Mavura, alimwelekeza aende Hospitali ya Hindu Mandal kutokana na kuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya upasuaji.

Aliendelea kudai kuwa Julai 9, 2018, Dk. Mavura alimfanyia upasuaji katika koo lake na alitoa sampuli za tezi la kushoto zikapelekwa katika Hospitali ya TMJ kwa ajili ya uchunguzi ambayo ilitoa ripoti yake ikidai kuwa alikuwa na ugonjwa wa Rapillary Carcinoma of Thyroid.

Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo Dk. Mavura alimfanyia upasuaji wa pili na kuiondoa tezi iliyoambukizwa ugonjwa huo. Sampuli zilipelekwa katika Hospitali ya TMJ kwa ajili ya uchunguzi mwingine na ripoti ilionesha tezi hizo zipo sawa hazina ugonjwa wowote.

Florence alidai, alichukua majibu hayo hadi Hospitali ya Hindu Mandal na alipofika aliambiwa amekutwa na kansa ya Thyroid na anatakiwa aende katika Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya kuanza matibabu ya mionzi.

Aliendelea kudai kuwa aliamua kuchukua uamuzi wa kwenda Hospitali ya Apollo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na madaktari walibaini tezi ya kushoto inayosaidia kutengeneza homoni imeondolewa wakati alipofanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Hindu Mandal.
L

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad