Mwanza. Mwanamke aliyeuwawa kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali na mwili wake kukutwa ukiwa umetelekezwa bondeni kwenye Mtaa wa Kuzenza eneo la Nyegezi jijini Mwanza, ametambulika kwa jina la Devotha Randa (37).
Marehemu Devother ambaye mwili wake ulikutwa bondeni Jumapili ya Septemba 4, mwaka huu ni mtoto wa Askofu wa Kanisa la Menonite Jimbo la Mwanza, Askofu Albert Randa.
Pamoja na jeraha shingoni, mwili wa marehemu Devother pia ulikutwa na majeraha maeneo ya usoni, kichwani, mikononi na miguuni.
Akizungumza na na Mwananchi jana nyumbani kwake, Mtaa wa Nsumba wilayani Ilemela, Askofu Randa, baba mzazi wa marehemu Devother alisimulia mazingira ya kifo cha mtoto wake kuanzia kutoweka nyumbani.
“Devother alikuwa anafanya kazi zahanati binafsi ya Juwa/Lavie eneo la Nyakato jijini hapa na Septemba 3 alikwenda kazini Saa 12:00 asubuhi na alitarajiwa kurejea nyumbani Saa 12:00 jioni; lakini hakurejea baada ya kutoa taarifa kuwa anamshikia mwenzake zamu ya usiku.
“Tulitarajia arejee nyumbani asubuhi ya siku iliyofuata ,lakini hakurejea na tulipopiga simu kazini tulitaarifiwa alishatoka na simu yake ilikuwa haipatikani. Hali hiyo ilitufanya tuingiwe wasiwasi na kuanza kumtafuta maeneo mbalimbali ikiwemo vituo vya polisi bila mafanikio,”alisema.
Alisema Septemba 5, familia iliamua kwenda chumba cha kuhifadhi maiti kwenye Hospitali ya Bugando, baada ya kupata taarifa ya mwili wa mwanamke asiyejulikana kukutwa bondeni eneo la Nyegezi na kubaini kuwa ni mwili wa mpendwa wao.
Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi, Askofu Randa alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwenda kijiji cha Roce wilayani Rorya ambako mazishi yatafanyika Septemba 16.
Mama anavyomkumbuka mwanaye
Akimzungumzia binti yake mama mzazi wa marehemu Devotha, Julitha Randa alisema milele atamkumbuka mwanaye kwa ucheshi, moyo wa kujitolea na kuwajali.
Alisema licha ya huzuni iliyoikumba familia kutokana na mazingira na kifo cha mtoto wake, bado anamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na kumwachia alama kupitia kwa wajukuu zake watatu aliomuachia.
“Nitawatunza na kuwalea kadri ya uwezo wangu”aliahidi Julitha.
Mtoto amlilia mama
Grace Elfas (19), mtoto wa kwanza wa marehemu Devother aliiomba Serikali kupitia mamlaka husika kukichunguza, kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Mtoto huyo anayesoma Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) eneo la Nyakato jijini Mwanza alisema japo marehemu mama yake ndiye aliyekuwa nguzo kuu ya maisha na elimu yake na wadogo zake, anaamini babu, bibi, ndugu na jamaa waliobaki watawahudumia na kuwasaidia kufikia malengo yao kielimu na kimaisha.