Bangala: Ibenge atatusamehe tu



Dar es Salaam. Nyota wa Yanga, Yannick Bangala, amewatumia salamu mashabiki wa klabu hiyo kuwa atasahau uhusiano wake na kocha wake wa zamani, Florent Ibenge wa Al Hilal ya Sudan.

Bangala alisema licha ya kujua ubora wa kocha Ibenge, lakini safari hii itakula kwake kwa vile Yanga imepania jambo moja tu, kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wao wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Agfika ili watinge hatua ya makundi.

Nyota huyo kutoka DR Congo, ambaye ubora wake uwanjani wa kucheza nafasi nyingi umempa jina la ‘Mzee wa Kazi Chafu’, aliliambia Mwananchi kuwa, kitu kilichopo akili mwa wachezaji ya Yanga sasa ni kutinga makundi mbele ya Al Hilal ya Sudan watakaovaana wikiendi ijayo.

Bangala alisema wanafahamu matajiri wa Sudan wapo chini ya kocha Ibenge, ambaye baadhi yao waliwahi kufanya naye kazi, lakini safari hii watakapokutana urafiki utawekwa pembeni.


“Tunafahamu kama wachezaji kuwa mara ya mwisho Yanga kucheza makundi katika Ligi ya Mabingwa ni mwaka 1998, tunataka kuirudisha timu hatua hiyo,” alisema Bangala, ambaye alichukua tuzo kubwa ya mchezaji bora wa msimu uliopita Yanga ikichukua makombe matatu bila kupoteza.

“Tunajua haitakuwa kazi rahisi, tunakutana na timu nzuri inayofundishwa na kocha ambaye alitulea Florent (Ibenge), tunamuheshimu sana, alitulea kama watoto wake, lakini kwa kukutana naye ni jambo la kawaida kwenye mpira, hatuwezi kuweka malengo yetu pemben,” alisisitiza Bangala.

Alisema jeuri kubwa juu ya kuishinda Al Hilal ni aina ya kikosi walichonacho msimu huu ambapo ongezeko la wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu pamoja na wao waliokuwepo tangu msimu uliopita ndiyo mtaji mkubwa kwao.


Yanga itaanza kucheza na Al Hilal kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Oktoba 8, kabla ya kurudiana na miamba hiyo wiki inayofuata nchini Sudan.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad