David Beckham akiwa katika foleni ya watu wa kawaida kuaga mwili wa Malkia Elizabeth II
NYOTA na Nahodha wa zamani wa Manchester United pamoja na Timu ya Taifa ya Uingereza David beckham alilazimika kusubiri kwenye foleni kwa muda wa masaa 12 ili kupata fursa ya kutoa heshima yake ya mwisho kwa Malkia Elizabeth II.
Beckham alionekana kwenye foleni hiyo akiwa pamoja na waombolezaji wengine ambao ni wananchi wa kawaida huku akiwa amevalia suti pamoja na kofia nyeusi.
Akifanya mahojiano na Shirika la Utangazaji la Sky News masaa kadhaa baada ya kutoka katika tukio hilo alinukuliwa akisema:
“Siku hii ilikuwa lazima iwe siku ngumu sana, naungana pamoja na familia, na inapendeza sana kusikia Habari zake kutoka kwa watu waliopo hapa. Nilikuwa mtu mwenye bahati sana ambaye nilipata nafasi ya kujumuika katika hafla na Mheshimiwa Malkia, ni siku ya huzuni lakini pia ni siku muhimu ya kukumbukwa.” alisema Beckham.
Beckham amemuongelea Malkia Elizabeth II kuwa alikuwa kiongozi wa aina yake aliyependwa na watu wengi duniani kutokana na kuwepo kwa salamu nyingi za pole zilizotiririka kutoka katika kila kona ya dunia ambazo zote hizo zinaashiria ni kwa namna gani alivyogusa nafsi ya kila mtu katika enzi za utawala wake akiwa hai.