BEKI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Chippa United ya Afrika Kusini, Abdi Banda amesema kitendo cha kuitwa Taifa Stars, kimempa mzuka na kumuongezea kujiamini wa kuzidi kupiga mzigo nje ya nchi kwa vile ni muda mrefu alisahaulika kwenye timu hiyo ya taifa.
Banda, aliitwa na Kocha Hanour Janza kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya Libya, ikiwa ni baada ya kupita muda mrefu bila kuitwa tangu 2019 kutokana na sababu kadhaa ikiwamo majeraha.
“Huku kuna ushindani mkubwa, ili ucheze lazima ujitambue kujua kocha anataka ufanye nini katika dakika alizokuamini kumfanyia kazi, nashukuru Mungu nimekuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza, hivyo kuitwa Stars kumeniongezea morali ya juu zaidi,” alisema Banda na kuongeza;
“Najua kwenye nafasi yangu kuna wachezaji wengi wazuri ambao wangeweza kuitwa, hivyo kitendo cha kujumuishwa kimenifanya nifarijike na kuongeza kasi zaidi kwenye kazi zangu.”
Banda alijiunga na Chippa United, akitokea Mtibwa Sugar ambako alicheza msimu mmoja, alisema ana malengo ya kufanya makubwa kwenye soka la nje, akikiri kuna wakati aliyumba ndio maana alirejea nyumbani kujipanga.
Kabla ya kutua Chippa Banda amewahi kuzichezea pia Coastal Union, Simba za Tanzania na Baroka na Highlands Park zote za Afrika Kusini.