Jeshi la polisi mkoani Shinyanga limethibitisha tukio la bomu kutelekezwa na mtu asiyejulikana katika benki ya NMB tawi la Shinyanga.
Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema mtu huyo aliingia ndani ya benki hiyo kama mteja akiwa amebeba begi, na kwenda kulitelekeza katika moja ya meza zilizopo ndani ya benki hiyo.
Baada ya muda mfupi begi hilo lililotelekezwa lilionekana likitoa cheche za moto na ndipo mmoja wa watumishi katika benki hiyo ya NMB tawi la Shinyanga alijaribu kuzima cheche hizo bila ya mafanikio.
Ndipo mtumishi huyo aliomba msaada kwa vyombo vya ulinzi , ambavyo vilifanikiwa kulitegua bomu hilo na kulitoa nje ya eneo la benki.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) amezungumza kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi ambaye amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa suala hilo lipo kiusalama zaidi.
“Labda nikuambie hili limekaa kiusalama zaidi limetokea siku nne zilizopita, sio tukio la jana ,leo wala juzi ila limekaa kiusalama zaidi ili kutotisha wananchi.” amesema Kamanda Magomi