HEBU vuta picha, unaenda kufanya utalii kwenye bonde moja, ukifika huko unakuta mawe makubwa yakiwa yamesambaa kwenye bonde, lakini ukichunguza vizuri, unagundua kwamba kila jiwe limeacha alama nyuma kama lilikuwa linasukumwa kutoka umbali mmoja hadi mwingine.
Wenyeji wanakwambia kwamba hakuna mtu yeyote anayeyasukuma mawe hayo, bali huwa ‘yanatembea’ yenyewe watu wakiwa wamelala. Ni jambo lisilowezekana si ndiyo?
Basi kwa taarifa yako, hizi siyo stori za kusadikika, ni kweli kwenye bonde la mto Racetrack Playa lililobatizwa jina la Death Valley, California nchini Marekani kuna mawe makubwa, mengine yakiwa na uzito wa takribani kilo 350 ambayo yanajongea yenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote na kuacha alama nyuma yake.
Kwa miaka mingi, tukio hilo limekuwa likiumiza sana vichwa vya wanasayansi na watafiti wa masuala ya miamba, na wakati huohuo pia eneo hilo limekuwa kivutio cha watalii kwa kipindi kirefu sana.
Kwa wastani, kila jiwe lina uwezo wa kuhama na kujongea kwa umbali wa mpaka mita 250, sawa na umbali wa viwanja viwili vya mpira na nusu vikiunganishwa.
Zipo imani nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na wenyeji kwa wageni wanaoenda kutembelea eneo hilo, imani iliyopata nguvu kubwa kwenye miaka ya tisini, ni kwamba mawe hayo huwa yanasukumwa na mizimu nyakati za usiku, wengine wamekuwa wakiamini kwamba viumbe kutoka sayari nyingine (aliens), ndiyo hufanya kazi hiyo kila siku.
Wapo wengine ambao wamekuwa wakiamini kwamba nguvu za kishetani zisizoonekana ndiyo husogeza mawe hayo, jambo lililofanya watu mbalimbali wanaoamini katika imani za kishirikina, kulitumia bonde hilo kwa ajili ya ibada za kishirikina.
Miaka mingi baadaye, hatimaye sababu za kisayansi kuhusu mawe hayo kujongea na kuacha alama nyuma, zimepatiwa majibu.
Ralph Lorenz, mwanasayansi kutoka Shirika la Utafiti wa Masuala ya Anga la Marekani (NASA), baada ya utafiti wa muda mrefu, amekuja na majibu yafuatayo.
Mto Racetrack Playa, hufurika maji yenye nguvu ndani ya kipindi kifupi katika mwaka, vipindi vingine huwa ni vya baridi kali ambayo husababisha maji ya mto huo kuganda, na kipindi kingine huwa ni cha ukame ambapo barafu huyeyuka na kuwa maji, ambayo nayo hukaukaa na kuacha mawe na mchanga.
Sasa katika kipindi cha baridi, mawe hayo makubwa hugandiana pamoja na barafu, joto linapoanza, barafu huanza kuyeyuka kuanzia chini kuja juu, katika kipindi hiki ambacho barafu inayeyuka, chini yake huwa kunapita mkondo wa maji wenye nguvu, na kwa sababu barafu ina kawaida ya kuelea kwenye maji, huwa inajongea taratibu ikiwa imegandiana na mawe hayo na baadaye maji yanapokauka, huwa kila jiwe limehamishwa kwa umbali fulani na barafu.
Maji yanapokauka, alama za jiwe kuburuzika hubaki kwenye matope ya mto ambayo baadaye hukauka kabisa na kuziacha alama hizo bado zikiendelea kuwepo. Hiyo ndiyo siri iliyojificha nyuma ya mawe yanayotembea ya Mto Racetrack Playa.