Kufungiwa kwa Mwakinyo ni ishara kwamba pambano la marudiano na Smith kama likiwepo halitachezwa kwenye nchi hiyo au Marekani ambako Smith amefungiwa, bali kwenye nchi nyingine.
Bondia Hassan Mwakinyo amefungiwa kucheza nchini Uingereza, ikiwa ni siku kadhaa tangu alipozichapa na Liam Smith nchini humo na kupigwa kwa TKO, raundi ya nne.
Kwa mujibu wa Mtandao wa ngumi za Kulipwa wa dunia (Boxrec), bondia huyo amefungiwa na Bodi ya Ngumi za Kulipwa Uingereza (BBBC).
Taarifa hiyo haikueleza chanzo cha bondia huyo namba moja nchini kufungiwa kucheza nchini humo, ingawa pambano na Smith linaweza kuwa chanzo.
Hata hivyo uamuzi huo hautamuathiri Mwakinyo kucheza nchi nyingine duniani, kulingana na taratibu za ngumi za kulipwa.
Smith wakati anazichapa na Mwakinyo, alikuwa amefungiwa kuzichapa nchini Marekani na Bodi ya Ngumi za kulipwa ya nchi hiyo.
Hapa nchini, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliiagiza Kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBRC) kufanya uchunguzi wa matokeo ya Mwakinyo na Smith ya hivi karibuni, ingawa uamuzi wowote hautamuathiri bondia huyo kuendelea na majukumu yake ya ngumi kwenye nchi nyingine kulingana na taratibu za mchezo huo.
Rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa amesema suala la Mwakinyo hapa nchini wameiachia Serikali, ingawa Bodi ya Ngumi Uingereza ndiyo inapaswa kumchukulia hatua.
"Bodi hiyo kama haikupitisha malipo yake, basi ndiyo adhabu, hapa nchini tunaweza kumuadhibu kwa kutochukua kibali cha TPBRC, lakini kwenye matokeo hiyo hiko chini ya Waingereza," amesema.
Mdau wa ngumi, Emmanuel Mlundwa amesema bondia kufungiwa inategemea, kunaweza kuwa na sababu ya nje au ndani ya ulingo.
"Ukifungiwa nchi moja unaweza kucheza kwingine, lakini pia kuna sababu, huenda umepigwa wanataka kukupumzisha, au umefanya matukio mengine nje ya ulingo, hata hivyo kufungiwa kwenye nchi moja hakutamuathiri kucheza nchi nyingine," amesema