Bungeni: Serikali Yatangaza Kufuta Tozo



Serikali imeridhia kufuta na kupunguza viwango vya tozo za miamala ya kieletroniki, ili kupunguza mzigo wa tozo kwa jamii, kuchochea matumizi ya miamala kwa njia ya fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia utozaji wa tozo husika mara mbili kutokana na utozaji wake kuhusisha pande zote mbili za mtoaji na mpokeaji.


Akitangaza uamuzi huo Bungeni jijini Dodoma hii leo Septemba 20, 2022, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Wizara yake imefanya mapitio hayo na kusema pia wamefuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote).


Amesema, “Wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa kusamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi shilingi 30,000 na kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50, kufuatana na kundi la miamala.”


Waziri Mwigulu ameongeza kuwa, “Viwango vya tozo vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha shilingi 10,000 hadi kiwango cha juu cha shilingi 7,000, viwango ambavyo vilianza kutumika tarehe 07 Septemba, 2021, Mheshimiwa Spika, marekebisho haya yataanza kutumika tarehe 1 Oktoba 2022.”


Aidha, amesema Serikali inafuta utaratibu wa kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utaratibu utakao bainishwa kwenye kanuni.


Ameongeza kuwa, “Napenda kusisitiza kuwa kodi ya zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya kupangisha,”amesema.


Hata hivyo, Waziri Mwiguli ameelekeza fedha hizoz ifidiwe kutokana na kubana matumizi mengineyo ndani ya Serikali, ambayo hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya msingi husika huku akimwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kukaa na maofisa kuangalia upya mafungu ya matumizi mengineyo.


Aidha amesema, “Tukate kwenye chai, vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na nje kwa maafisa wa wizara zetu kama Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) alivyoelekeza, tukate mafunzo, semina, matamasha, warsha.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad