Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM) imeielekeza Serikali kuchukua ushauri wa wananchi kuhusu tozo sambamba na kujielekeza katika kubana matumizi ya serikali na kutanua wigo wa kodi.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Septemba 8, 2022 jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumzia maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichokaa jana Septemba 8, 2022 kikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
CCM imeingilia kati tozo siku chache baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba pamoja na mawaziri wenzake kujitokeza kuzungumzia tozo wakati kukiwa na malalamiko ya wananchi na wadau wengine kuhusu tozo hizo.
Shaka amesema Kamati Kuu imewapongeza Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kazi nzuri wanayoifanya na pia kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya uchaguzi.
Amesema Kamati Kuu inatambua mafanikio yaliyofikiwa kutokana na mapato ya tozo kama vile ujenzi wa vituo vya afya 234 pamoja na sekondari 214.
Hata hivyo, imeielekeza Serikali kutazama hali halisi na kuchukua maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki.
"Kamati Kuu ya halmashauri kuu ya CCM Taifa umeielekeza Serikali kutazama hali halisi na kuchukua hatua stahiki kuhusu maoni na ushauri wa wananchi kuhusu tozo.
"Kamati Kuu ya CCM imeielekeza Serikali kufikiria na kujielekeza katika kubana matumizi ya Serikali lakini pia kuendelea kujenga mazingira rafiki na wezeshi ili kujenga uchumi imara unaozalisha kwa lengo la kutanua wigo wa kodi pamoja na kubuni vyanzo vipya vya kodi ili kuwa na viwango na mfumo rafiki wa kodi kwa kila mmoja," amesema Shaka.
Shaka amewataka wasaidizi wa Rais Samia washuke chini kwa wananchi ili kusikiliza shida zao sambamba na kujua hali halisi ya maisha yao.
"Tunafuatilia mwenendo na uwajibikaji wa wateule wote wa Rais. Chama ndiyo mwenye mali, kwa hiyo lazima tuimamie serikali," amesema Shaka wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari katika Ofisi Ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini hapa.