CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekoleza moto kuhusu kilio cha tozo za miamala ya kielektroniki huku kikitaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kuachia ngazi au atumbuliwe.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amesema kutokana na suala hilo kuzidi kulalamikiwa na wananchi, ni vyema Dk. Nchemba akajiuzulu au Rais Samia Suluhu Hassan atengue uteuzi wa waziri huyo kwa kuwa ameshindwa kuchukua hatua sahihi za kisera kwa wakati sahihi kuhusu tozo.
Pia amesema waziri huyo anapaswa kusitisha mara moja kanuni za viwango vya tozo za miamala ya kibenki na kanuni nyingine kandamizi zinazohusu miamala ya kielektroniki.
Katika taarifa iliyotolewa jana, Mnyika alisema ni muhimu kwa serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, ikiwamo kuachana na kununua magari ya kifahari ya kila taasisi, mamlaka za serikali za mitaa na watendaji wengine ambayo hayana umuhimu kwa taifa.
“Kuunda tume kwa ajili ya tozo ni matumizi mabaya ya fedha za umma, ni kuendelea kuwabebesha wananchi maumivu ya tozo kwa muda mrefu zaidi. Waziri wa Fedha (na Mipango) anapaswa kujiuzulu au Rais kutengua uteuzi wake,” alisema Mnyika.
“Baada ya kusitisha, suala ambalo anaweza kufanya hata leo, upatikane ufumbuzi wa kudumu kwa kupeleka bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Fedha katika mkutano wa Bunge ulioanza leo (jana), ili kuepusha madhara ya muda mrefu na ya baadaye kwa nchi na wananchi kutokana na kasoro hizo za kisheria,” alisema.
Mnyika alisema kuwapo kwa tozo hizo kumeathiri uchumi wa nchi pamoja na mzunguko wa fedha katika mfumo rasmi na hivyo kutishia uwapo wa uhai wa taasisi za kifedha.
“Watanzania walio wengi wanafanya uamuzi wa kuachana na utaratibu wa kuweka fedha au akiba kwenye mfumo rasmi kutokana na makato ya tozo ambazo zimeanzishwa na serikali baada ya sheria ya fedha kutungwa na bunge. Tozo hizi zinatozwa bila kujali kuwa wananchi walishalipia kodi ya mapato yao,” alisema Mnyika.
Alitaja baadhi ya athari za tozo kwa wananchi kuwa ni pamoja na kuua ongezeko la watu kwenye mfumo rasmi wa kifedha jambo ambalo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi kutokana na watu kuanza kutumia njia zisizo rasmi kuhifadhi fedha zao.
Alisema tozo hizo zinaathiri mishahara na pensheni ambazo zinapitia katika mfumo rasmi wa kibenki ambazo tayari zilishakatwa kodi, lakini zinatozwa tena kwenye mapato ambayo tayari yalishakatwa.
Athari nyingine alisema tozo zinapunguza nguvu za mtu mmoja mmoja katika kufanya manunuzi hususani wale ambao kipato chao hakiongezeki ikiwamo wastaafu.
“Wastaafu wanalazimika kulipa tozo kwenye mapato ambayo walishalipia kodi awali, huku ni kuwafanya wawe maskini na fukara zaidi,”alisema Mnyika na kuongeza kuwa tozo pia zinapunguza mzunguko wa fedha kwenye uchumi, hivyo kuathiri uzalishaji, na kwamba zinasababisha serikali kukosa mapato ya kodi.
“Mathalani kuna kampuni ambazo zimetangaza kupata hasara kutokana na wananchi kuamua kutokutumia mifumo rasmi ya kifedha. Tozo zisipodhibitiwa zitakuwa na athari kubwa kwenye taasisi za kifedha hasa benki kwa sababu wananchi wataamua kuwa na utaratibu wa kutunza fedha zao kwa mifumo ambayo sio rasmi, jambo ambalo litaudidimiza uchumi wa taifa,” alisema Mnyika.
Alishauri kwamba ni vyema kuachana na utaratibu wa tozo na kurejea kwenye utaratibu wa awali pamoja na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa serikali.
Pia alishauri kufanyike tathmini ya kina kujua faida na hasara za kuendelea na miradi mikubwa na mikataba ambayo serikali ya awamu ya sita imeiridhia ambayo haina msisimko wa kiuchumi na ambayo feza zote zinafanya manunuzi nje ya nchi na hivyo kusababisha mzunguko wa fedha kuwa mdogo.
Aidha, alishauri serikali kupunguza mikopo mikubwa ya kibiashara kwa ajili ya kujiendesha badala yake ikope kwa ajili ya miradi ya maendeleo na si kwa ajili ya miradi ambayo haisisimui uchumi wa taifa .
Mnyika alishauri ifanye uamuzi wa kuwezesha sekta binafsi katika kufanya biashara badala ya kuendelea kuendesha biashara ambazo inapata hasara kama vile miradi ya kuzalisha umeme na reli.
Pia ianzishe vyanzo vipya vya mapato kwenye sekta za uvuvi wa bahari kuu, kupanua wigo wa uzalishaji kwenye kilimo ili kujitosheleza kwa chakula pamoja na kuuza nje ya nchi.