Dar es Salaam. Wakati Chadema ikiendelea na mazungumzo na Serikali na CCM, Kamati Kuu ya chama hicho imetoa masharti manne ya kuzingatiwa ili kiendelee na mazungumzo hayo.
Masharti hayo ni kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani, kukamilishwa kwa mchakato wa katiba mpya, kuondolewa kwa wabunge 19 wa Viti Maalum bungeni na kuundwa kwa kamati ya pamoja ya wataalamu wa sheria ili iandae maboresho ya kisheria yatakayohusishwa katika mabadiliko ya Katiba.
Masharti hayo yametolewa kupitia Kikao cha Kamati Kuu iliyoketi Septemba 17 na 18, 2022 jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa ya kikao hicho leo Jumanne Septemba 20, 2022, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kuhusu Katiba mpya, kamati hiyo imeazimia kuandaliwa kwa muswada wa sheria ya utekelezwaji na upelekwe bungeni kabla ya kikao cha bunge cha Novemba,2022.
“Muswada huo unatakiwa kutolewa wazi sio kinyemela, ili watu waone na watoe maoni yao,” amesema Mwalimu.
Sharti lingine lililotolewa na Kamati Kuu hiyo ni kuondolewa bungeni kwa wabunge 19 wa viti maalum wa chama hicho, akisisitiza hilo lifanyike kabla ya kikao cha bunge cha Novemba, 2022.
Hata hivyo wabunge hao akiwemo Halima Mdee na wenzake wamefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.
Mdee na wenzake wamevuliwa uanachama wa chama hicho Novemba 27, 2020 kwa sababu wamekiuka katika na kanuni za chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila chama hicho kuwapitisha.
Kulingana na Mwalimu, sharti lingine ni kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa vya upinzani, bila masharti.
Kadhalika, kimetaka kuundwa kwa kamati ya pamoja ya wataalamu wa sheria ili iandae maboresho ya kisheria yatakayohusishwa katika mabadiliko ya Katiba.
Hata hivyo, amesema chama hicho kimeshatoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi za chini kuandaa mikutano ya hadhara itakayofanyika nchi nzima kwa kufuata kanuni na sheria zilizopo sasa.