Dejan atoa sababu tatu, sinema nzima ilikuwa hivi...




‘KWAHERI Mzungu...Kwaheri Mzungu...ndio kibwagizo kilichosikika mchana wa jana wakati, straika wa Simba, Dejan Georgijevic alipowasili Bandarini Jijini Dar es Salaam, akitokea visiwani Zanzibar, akiwa katika harakati za kurudi kwao Serbia baada ya kutangaza kusitisha ghafla mkataba na klabu hiyo.

Straika huyo kutoka Serbia, ameondoka nchini kurudi kwao ikiwa ni siku 52 tangu kuanza kazi Simba Agosti 7. Amedai kusitisha mkataba kwa kukiukwa kwa baadhi ya vipengele alivyokubaliana na klabu hiyo, huku akitaja sababu kuu tatu.

PICHA LILIVYOANZA

Saa 5:30 asubuhi alituma ujumbe kwenye grupu la WhatsApp la wachezaji akiwaambia anaondoka kwenye timu na kwamba anayetaka kumuaga amfuate kwenye kantini ya hotelini waliyopo. Mastaa wengi wakaenda kumuaga.

Dakika chache badae akalefti na kuposti kwa mashabiki kupitia akaunti yake ya Instagram kwamba ameachana na Simba. Ilipofika saa 6 mchana jamaa akabeba mabegi yake mawili na kupanda boti kurudi Dar.


Saa 2 na nusu zilimtosha Dejan kutua Dar na kupokewa na mashabiki saa 8:30 mchana bandarini na kisha alikwenda ofisi za Simba kukamilisha taratibu zake za kumalizana na timu hiyo ili kutimkia Serbia, mipango ilkuwa aondoke usiku wa kuamkia leo. “Nathibitisha kuwa mkataba wangu na Simba umevunjika, kutokana na kukiukwa makubaliano ya kimkataba, asante mashabiki kwa mapenzi yenu.”

SABABU

Mwanaspoti limeambiwa sababu ya kwanza iliyomuondoa Dejan Simba ni kwamba tangu alipofika nchini Agosti 7, alikuwa akiishi katika moja ya hoteli kubwa iliyopo Mbezi baada ya kushindwa kupata nyumba ya kuishi iliyokuwa na vigezo vyake kwani kila alipokuwa akienda kukagua alipakataa.

Sababu ya pili Dejan ni kutokana na kushindwa kupatiwa baadhi ya stahiki zake walizokubaliana na uongozi wa Simba kwa wakati tangu anasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo.


Miongoni mwa maslahi hayo ni mshahara wake, bonasi pamoja na pesa ya usajili.

Sababu ya tatu ni kutoridhishwa na hali ya mambo kwa ujumla ndani na nje ya uwanja yalivyokuwa yanaendelea ndani ya timu hiyo.

MSIKIE YEYE

Akiwa Bandari ya Dar, mara baada ya kurejea aliliambia Mwanaspoti si vyema kuweka wazi sababu zilizochangia kufanya maamuzi hayo ila kuna mambo hayakwenda sawa kwenye makubaliano yao ya mkataba na uongozi.

Dejan alisema kuna vitu alikubaliana na uongozi na kuelezwa atapatiwa ila kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda aliona hakuna ambalo limetimizwa.


Alisema Simba ni timu kubwa Afrika si vyema kuweka wazi mambo hayo ila ndio vitu vikubwa vilivyochangia kufanya maamuzi ya kurudi kwao Serbia kwa ajili ya kujipanga kabla ya kuanza maisha mengine.

“Maisha ya mpira ndio yalivyo kuna maamuzi magumu lazima yafanyike kwa ajili ya hatma ya maisha yangu nawapa pole mashabiki wa Simba, naipenda timu hii ila ilikuwa haina jinsi kufanya maamuzi hayo,” alisema staa huyo ambaye inatajwa huenda akaibukia Saudi Arabia.

SIKU 52 SIMBA

Katika siku hizo 52, timu ilicheza mechi saba za kimashindano Ngao ya Jamii moja, Ligi Kuu Bara mechi nne na mbili Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alicheza nne, hakuanza kikosi cha kwanza na yote alikuwa akiingia kipindi cha pili. Jumla ya dakika alizocheza katika michezo yote minne ni 70, hata dakika za kwenye mchezo mmoja ambazo ni 90, hakuzifikia licha ya kuwa kipenzi cha mashabiki.


Katika Ligi Kuu Bara Dejan alifunga bao moja dhidi ya Kagera Sugar ambao Simba ilishinda mabao 2-0, lingine likifungwa na Moses Phiri.

MENEJA WA SIMBA

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema si vyema kumzungumzia mchezaji mmoja kutokana na maamuzi yake binafsi ambayo aliamua kuyafanya. Hakuna kiongozi yoyote wa Simba aliyekubali kufafanua sakata hilo hadi tunakwenda mitamboni.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad