Diamond Platnumz; ni msanii mkubwa wa muziki barani Afrika akiiwakilisha vyema Nchi ya Tanzania ambaye kuna baadhi ya watu wanadai kuwa huyu wa sasa si yule wa miaka minne au mitano iliyopita.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya burudani wanasema kuwa, ubora wa Diamond au Simba kwenye eneo la kimataifa umeshuka ukilinganisha na miaka hiyo.
Wapo wanaosema kuwa, ukitaka kujua hilo, tazama kolabo zake na wasanii wakubwa wa kimataifa ambazo zimepungua mno.
Wapo wanaosema kuwa, mpaka sasa ukitaja wasanii kumi bora Afrika katika jicho la kimataifa zaidi; kwa maana ya wale wanaofanya kolabo nyingi na wasanii wakubwa nje ya Bara la Afrika, huwezi kumtaja Diamond au Mondi.
Wanasema kuwa, ni kama vile milango ya nje imekuwa migumu kufunguka kwa Diamond tofauti na Wizkid, Burna Boy na sasa hata wasanii wapya wa Nigeria, Rema, Ayra, Fireboy na wengine wanapiga bao kwenye eneo hilo.
Wanadai kwamba, ni kama ushawishi wa Diamond kwenye mitandao mikubwa kama YouTube umeshuka kwa kiasi f’lani.
Mifano inayotolewa ni ile ya kulinganisha nyimbo zake za zamani za Yope Remix, Waah, Inama, Sikomi na nyingine ambazo zimevuna wasikilizaji na watazamaji mamilioni, lakini za sasa kutoka kwenye Ep yake ya FOA hazilingani na za enzi hizo.
Wapo wanaodai kwamba, jambo lingine linaloonesha kuwa, Simba wa sasa siyo yule aliyekuwa anatisha pengine kuliko mnyama yeyote, ni kitendo cha kupambanishwa na kijana wake, Harmonize ambaye hakauki kwenye midomo ya mashabiki wake kama alivyokuwa Diamond wa kipindi cha Wema Sepetu, Zari The Boss Lady, Hamisa Mobeto na Tanasha.
Wanasema kuwa, huyu Diamond wa Zuchu siyo yule!
By 2Jiachie