EXCLUSIVE: Kisinda afunguka kilichomrudisha Yanga, Kambole



WINGA mwenye kasi zaidi, Tuisila Kisinda ‘TK Master’ amechekelea kukamilika kwa usajili wake wa kurejea Yanga akisema anarudi nyumbani kupiga kazi na kuendeleza moto aliouacha, huku mabosi wa Yanga wakiendelea kufanya usiri juu ya jina la nyota mmoja wanayemkata kumpisha winga huyo.

Kisinda aliyeuzwa na Yanga msimu uliopita kwa Klabu ya RS Berkane ya Morocco, lakini akashindwa kuwika kama alivyokuwa Jangwani na sasa amerejea kama Mwanaspoti lilipowahabarisha juzi Alhamisi likiwa gazeti pekee lililonasa usajili huo wa dakika za mwishoni kabla dirisha la usajili halijafungwa rasmi.

Kutua kwa Kisinda kumelifanya benchi la ufundi kukuna vichwa juu ya nyota gani wa kuwapisha ili kukidhi mahitaji ya kanuni ya usajili wa wachezaji wa kigeni inayoitaka kila klabu kuwa na wachezaji 12. Kwa sasa Yanga ina nyota 13.

Hata hivyo, habari za ndani zinasema jina na Lazarous Kambole ndilo limeondolewa, huku Jesus Moloko na Heritier Makambo wakipenya kwenye tundu la sindano.


Inadaiwa Kambole ni majeruhi wa muda mrefu.Japokuwa bado mabosi wa klabu hiyo wamekuwa na usiri kutokana na kuwepo kwa mgawanyiko wa watu wa kuachwa.

Mwanaspoti juzi mchana lilimtafuta Kisinda akiwa Morocco akijiandaa kuja nchini kuungana na kikosi hicho na kuzungumza naye ambapo alisema alikuwa katika wakati mgumu kama dili lake la kurejea Yanga lingekwama, lakini sasa ana amani ya roho kurudi nyumbani yaani Jangwani.

Kisinda anayekubalika kwa mashabiki wa Yanga na kuuzwa kwake RS Berkane kuliwavuruga kwa kukosa ule udambwidambwi wake wa kuwakimbiza mabeki wa timu pinzani, alisema ingawa AS Vita imemsaidia kuonekana, lakini Yanga imemtambulisha kwa nafasi kubwa kuanzia siku ya kwanza alipofanyiwa mapokezi makubwa na hilo limemfanya kuamini Jangwani ni kama nyumbani kwake.


“Nimezitumikia Union Maniema na AS Vita za DR Congo, lakini Yanga imenipa jina kubwa zaidi na sio tu kwa kuwafanyia kazi nzuri, ila nikikumbuka siku ya kwanza tu walivyonipokea haraka nilikuwa mchezaji mkubwa,” alisema na kuongeza;

“Isingekuwa rahisi kukataa kurudi Yanga, ndiyo imenipa jina kubwa hata sasa nikafika hapa Morocco, nilikuwa katika wakati mgumu nikiomba hii hatua ya kurejea Yanga ikamilike. Sasa narudi Yanga, narudi Tanzania nakuja kuendeleza kazi niliyoishia katikati, nakwenda kuungana na familia yangu kushirikiana nao.”

Kisinda ambaye ana medali ya Kombe la Shirikisho Afrika aliyochukua msimu uliopita akiwa na RS Berkane alisema anaamini anakwenda kukutana na Yanga iliyokamilika zaidi.

Winga huyo aliongeza zaidi alisema anataka kuhakikisha anaisadia Yanga kutetea mataji yake lakini zaidi anataka kuhakikisha anaisaidia klabu yake hiyo kufanya vitu bora kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.


“Yanga hii ni kubwa tofauti na ile ambayo niliiacha ina, siwezi kucheza kwa kutumia kazi niliyofanya nyuma narudi na akili ya kufanya juhudi kubwa ili nipate nafasi ya kucheza.

“Niliongea na kocha (Nasreddine Nabi) ameniambia anachotaka na nitapambana kwa ajili ya timu, mashabiki wa Yanga wasubiri nakuja kuwafurahisha zaidi.”


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad