FISTON Mayele na Moses Phiri wana kazi nzito mbele yao ya kuhakikisha timu zao zinatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuzivusha katika raundi ya kwanza lakini ikiwa hilo litafanikiwa, watabakia na jukumu lingine zito la kuwezesha timu zao kuvuna zaidi ya Sh 9.4 bilioni kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
FISTON Mayele na Moses Phiri wana kazi nzito mbele yao ya kuhakikisha timu zao zinatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuzivusha katika raundi ya kwanza lakini ikiwa hilo litafanikiwa, watabakia na jukumu lingine zito la kuwezesha timu zao kuvuna zaidi ya Sh 9.4 bilioni kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kiasi hicho cha fedha ni kile ambacho bingwa wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu atapata kutoka CAF baada ya mabadiliko ya zawadi kwa washindi wa mashindano hayo na yale ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuongeza kiwango cha fedha za zawadi tofauti na kile cha msimu uliopita.
Mwanaspoti limeambiwa na chanzo cha uhakika ndani ya Kamati ya Utendaji ya CAF kwamba kuanzia msimu wa 2022/2023 na kuendelea, bingwa wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, atapata kitita cha Dola 4milioni (Sh9.3 bilioni) ikiwa ni ongezeko la Dola 1.5 milioni (Sh3.5 bilioni) kutoka kiasi ambacho bingwa wa msimu uliopita alipata kwa kutwaa taji la mashindano hayo.
Bingwa wa msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambaye ni klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, alipata kiasi cha Dola 2.5 milioni (Sh 5.9 bilioni), kiwango cha fedha ambacho ndio kilikuwa kinatolewa na bingwa wa kila msimu kwa muda wa misimu sita mfululizo.
Ongezeko hilo kubwa la fedha za zawadi kwa bingwa wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu limechangiwa na ongezeko la fedha za jumla za zawadi kwa washindi wa nafasi mbalimbali katika mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya Klabu Afrika lililoamriwa na Kamati ya Utendaji ya CAF.
Tofauti na awamu iliyopita ambapo fedha za jumla za zawadi kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilikuwa ni kiasi cha Dola 12.5 milioni (Sh29 bilioni), kuanzia msimu huu, fedha za jumla kwa washindi wa mashindano hayo ni kiasi cha Dola 17.6milioni (Sh41 bilioni) ikiwa ni ongezeko la Sh12 bilioni.
Lakini sio tu bingwa ambaye atanufaika na ongezeko la fedha bali pia kutakuwa na ongezeko la fedha za zawadi kwa timu itakayomaliza katika nafasi ya pili, zitakazoishia nusu fainali, robo fainali na zile ambazo zitakwama katika hatua ya makundi.
Inatajwa kuwa huenda kukawa na ongezeko la kiasi cha Dola 100,000 (Sh235 milioni) au Dola 200,000 (Sh470 milioni) katika kiwango cha awali kilichokuwa kinatolewa kwa timu zinazoishia hatua ya makundi ama robo fainali na nusu fainali.
Kwa awamu iliyopita, timu inayoishia hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika ilikuwa ina uhakika wa kuvuna Dola 550,000 (Sh 1.3 bilioni), wakati inayoishia robo fainali ilikuwa ikipata kiasi cha Dola 650,000 (Sh 1.5 bilioni.
Timu inayoishia hatua ya nusu fainali ilikuwa ikipata kiasi cha Dola 850,000 (Sh 2 bilioni) wakati inayomaliza katika nafasi ya pili ilikuwa ikivuna kiasi cha Dola 1.25 milioni (Sh 2.9 bilioni).
Lakini pia ongezeko hilo huenda lisizinufaishe Simba na Yanga tu bali pia Azam FC na Kipanga zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika ambalo nalo limeongezewa kiasi cha jumla cha fedha za zawadi kwa washindi wake kuanzia timu itakayotwaa ubingwa hadi itakayoishia hatua ya makundi.
Wakati awamu iliyopita fedha za jumla za washindi kwa Kombe la Shirikisho zilikuwa ni Dola 6.375milioni (Sh14.9 bilioni), kuanzia msimu ujao, fedha zitakazotumika kugawanywa kwa washindi zitakuwa ni kiasi cha Dola 9.9 milioni (Sh23 bilioni).
Straika wa Yanga, Fiston Mayele alisema kuwa ongezeko la kiwango hicho cha fedha linawapa hamasa zaidi ya kuhakikisha timu yao inafanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
“Sisi wachezaji tunajiandaa kikamilifu kuhakikisha malengo tuliyojiwekea ya kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanatimia. Tunachowaomba mashabiki ni kutuunga mkono kwa kuanzia mechi yetu dhidi ya Al Hilal. Wajitokeze kwa winmgi kutusapoti tupate ushindi na kuingia hatua ya makundi na baada ya hapo tutapambane kumaliza hatua za juu zaidi,” alisema Mayele