LICHA ya kutoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Geita Gold imetupwa nje ya kombe la Shirikisho Afrika kwa kanuni ya bao la ugenini kufuatia mchezo wa kwanza Sudan kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Hilal Alsahil.
Katika mchezo huo ambao umechezwa kwenye uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Alsahil ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tano kabla ya wachimba dhahabu hao wa Geita kusawazisha kipindi cha pili.
Geita Gold ilipata bao la kwanza kupitia kwa Daniel Lyanga kabla ya Edmund John kufunga la pili na ushindi, matokeo ya jumla ni sare ya mabao 2-2 lakini wawakilishi hao wa Tanzania wametupwa nje kwa kanuni ya bao la ugenini ambalo Wasudan wamepata.
Huu ulikuwa msimu wa kwanza kwa Geita Gold kushiriki michuano ya kimataifa kufuatia msimu uliopita kushika nafasi ya nne Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wachimba madini hao wanakibarua cha kurejea tena msimu ujao kwenye michuano hiyo kwa kufanya vizuri kwenye ligi msimu huu wa 2022/23.