Dar es Salaam. Italeta ahueni ndivyo unavyoweza kueleza, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo kutangaza bei mpya za ukomo wa mafuta kwa Septemba zitakazoanza kutumika kesho Jumatano.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Septemba 5, 2022 na Mkurungenzi Mkuu wa Ewura, Modestus Lumato bei za mafuta zimeonekana kupungua baada ya kupanda mfululizo kwa miezi mitano kuanzia Aprili mwaka huu.
Hadi leo katika mkoa wa Dar es Salaam bei ya petroli inaonyesha inauzwa kwa Sh3, 410 kwa lita, dizeli Sh3, 322 na mafuta ya taa yakiuzwa Sh3,765 kwa lita.
Lakini kuanzia kesho Jumatano petroli itauzwa kwa Sh 2, 969, dizeli Sh3, 125 na mafuta ya taa yatauzwa Sh 3,335 bei hizi ni kwa mkoa wa Dar es Salaam baada ya ruzuku ya Serikali.
Kwa mujibu wa Lumato, kushuka kwa bei za bidhaa hizo kunatokana na kupungua kwa bei za mafuta katika soko la dunia ya mwezi Julai ambayo mafuta yanayotumika kuanzia kesho yamenunuliwa mwezi huo.
“Bei za mafuta katika soko la dunia za Julai 2022 zimepungua ikilinganishwa na bei hizo kwa Juni 2022.
“Hivyo, bei za mafuta katika soko la ndani zimepungua vilevile kwa kati ya Sh 271 kwa lita na Sh362 kwa lita kwa petroli na kwa Sh430 kwalita kwa mafuta ya taa ukilinganisha na bei zenye ruzuku za Agosti 2022.
Kuhusu bei ya dizeli taarifa hiyo ilieleza, “Kwa mafuta ya dizeli, ukiiacha bei ya Tanga ambayo inashuka kwa Sh13 kwa lita, bei za Septemba 2022 zimeongezeka kwa Sh37 kwa lita na Sh 86 kwa lita kwa Dar es Salaam na Mtwara, ukilinganisha na bei zenye ruzuku za Agosti 2022.
“Ili kuendelea kupunguza madhara ya ongezeko la bei za dizeli hapa nchini ambapo shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea dizeli na pia ili kupunguza tofauti kati ya bei za petroli na dizeli, Serikali imetoa ruzuku ya Sh65 bilioni ili kupunguza bei za mafuta za Septemba 2022.