Hatimaye Mwakinyo Afunguka A to Z Sakata la Kuuza Mpambano na Kukosa Milioni Mia Nane

 


Wengi wameshuhudia dakika 10:49 za Hassan Mwakinyo na Liam Smith ulingoni, huku Watanzania wengi wakishangazwa na kilichotokea hadi, bondia huyo namba moja nchini kupigwa kwa Technical Knock Out (TKO) usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita licha ya yeye ndiye kuonekana amecheza vizuri na kuongoza raundi ya pili.

Kila mmoja anazungumza lake kuhusu pambano hilo lililopigwa Uingereza, wengine wakihisi kama ameliuza, wengine wakichukulia ni hali ya mchezo, na wengi wakishangazwa na namna lilivyokwisha, nyuma ya pazia Mwakinyo amefichua changamoto alizopitia kwenye maandalizi hadi kucheza pambano hilo lililopigwa mjini Liverpool.


“Wengi hawafahamu niliyopitia, nimepitia changamoto nyingi, nyingine hata siwezi kuzisema kwa kuwa pambano limepita, kuna watu wanasema nimeuza pambano ambalo kama ningeshinda nilikuwa na pambano jingine ambalo ningelipwa paundi 800,000, hivyo kwa Smith ningeuza pesa ngapi?


“Hivi kama kweli kama nimeuza pambano ni kiasi gani nimelipwa hadi niamue kuziacha paundi 800,000?,” alisema Mwakinyo katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti jana asubuhi.


KUMBE ALITAKA ASIPIGANE


Mwakinyo anasema kabla ya kuondoka nchini Agosti 31, alipanga asisafiri kwenda Uingereza kwenye pambano hilo lililokuwa la raundi 12 la uzani wa super welter.


“Kuna muda nawaona viongozi wengine wanazungumza kwenye mitandao ya kijamii kuhusu pambano langu, lakini baadhi yao kabla sijaondoka nchini nilikuwa nikiwapigia simu wanisaidie hawapokei,” anasema.


Anasema hadi Agosti 30 hakuwa amepata visa, alijaribu kila njia kuhakikisha anafanikisha hilo, bila mafanikio na watu aliotarajia wamsaidie hawakumpa ushirikiano.


“Nilitaka nisiende, kuna muda nilihisi pambano hilo halitachezwa, hadi Agosti 31 ndipo nilipata visa tena peke yangu, timu yangu kuanzia kocha na wengineo walikosa visa, awali nilitaka nisisafiri, lakini nikaambiwa taswira yangu itakuaje ukizingatia pambano limekwishatangazwa, nikalazimika kusafiri peke yangu,” anasema Mwakinyo kwa uchungu.


Anasema alisafiri usiku wa Agosti 31 na Septemba Mosi, saa 2 Asubuhi aliwasilia mjini Liverpool, ambako akiwa uwanja wa ndege ndipo alibaini begi lake halipo.


“Niliambiwa nisubiri hadi saa 5 asubuhi ili kupata begi langu, nilisubiri pale uwanjani, wakati huo sijala chochote, huku promota wa pambano naye anataka nikapime vipimo vyote siku hiyo hiyo.


“Wafanyakazi wa ndege waliniambia begi langu limesahaulika Amsterdam, lakini nikatakiwa tena nisubiri kwa saa tano zingine hili kulipata, wakanishauri niondoke na litakapofika watanijulisha kwa kuwa nilitakiwa kwenye vipimo haraka siku hiyo kama kanuni zinavyotaka,’.


Anasema tukio lile na kukosa visa kwa wakati, kutakiwa kwenye vipimo, hajapumzika na siku inayofuatia ana jukumu la kupima uzito, yuko peke yake kulimvuruga, na hadi siku ya pambano Septemba Mosi, hakuwa amepata begi lake, hivyo hata mazoezi mengine kule alifanya kwa tabu.


“Siku ya pambano nilivaa nguo ambazo sijazizoea, viatu ‘ring bout’ sivyo nilivyovizoea, kwa hali ya kawaida wengi wanaweza kuchukulia ni utetezi, lakini ni ngumu sana mchezaji kutumia vifaa ambavyo hujavizoea kwenye pambano, havikuweki huru, ndivyo ilikuwa kwangu,” anasema.


Anasema licha ya changamoto hiyo, lakini pia wasaidizi wa ulingo aliokuwa nao kwenye pambano lile hawakuwa watu ambao wamekuwa naye kwenye maandalizi.


“Siwezi kuwalaumu ma-second ‘wasaidizi wa ulingo’ nilokuwa nao kwa kuwa wale walikuwa wakinisaidia tu baada ya kuwa peke yangu kule, kama nilivyosema awali, timu yangu yote ilikosa visa, nikalazimika kusafiri peke yangu, hivyo wale walijitolea tu kunisaidia,”.


AKOSA PAMBANO TAMU


Mwakinyo anasema hadi kucheza na Smith amepitia changamoto nyingi ngumu ambazo nyingine hawezi kuzisema, lakini kinachomuumiza ni pambano la bei ghali zaidi ambalo alikuwa ameahidiwa na promota kama angeshinda.


“Niliambiwa kuna pambano la paundi 800,000, sharti lake ilikuwa ni kama tu ningempiga Smith, ndiyo sababu nilicheza kwa hali raundi za mwanzo, sikutaka kabisa kuacha lile pambano na Smith maana nilijua faida yake kwangu ni ipi, lakini moyo ulitaka nipambane, mwili ukanigomea,” anasema.


MALIPO DOLA 100,000


Katika pambano hilo inaelezwa Mwakinyo ameingiza kitita cha Dola 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh230 Milioni fedha ambazo anasema hata kama ni kweli amelipwa, lakini itabaki kuwa siri yake.


“Huwa sipendi kuzungumzia pesa ninayolipwa kwenye pambano, japo ni kweli nimelipwa pesa nzuri, lakini hata ikiwa ni kweli nimelipwa dola 100,000 au si kweli, bado itabaki kuwa siri yangu, nitaifanyia nini pesa hiyo pia itabaki kuwa siri yangu,” anasema.


KURUDIANA NA SMITH


Mwakinyo ambaye anasema alitaka ashinde pambano lile na hakuwa na fikra za kuacha na kuruhusu kipigo cha TKO, amekubaliwa na promota kuandaa pambano la marudiano kama ambavyo aliomba muda mfupi baada ya kushuka ulingoni.


“Promota amekubali, marudiano itakuwa ni baadae Januari, lakini haitakuwa tena kwenye mji wa Liverpool, itakuwa ni mji mwingine hapa hapa Uingereza.


“Namuomba mwenyezi Mungu atuweke hai, nijiandae vizuri, nisiwe na changamoto yoyote, nitawathibitishia Watanzania kwamba kilichotokea Septemba 3 ilikuwa ni bahati mbaya tu na huenda hata changamoto zote nilizokutana nazo hjadi siku napanda ulingoni zilipangwa zitokee ndiyo sababu nilipitia vikwazo vingi tangu nikiwa nyumbani hadi siku napanda ulingoni,” anasema.


ANARUDI BONGO 


Mwakinyo ambaye jana Jumatano anatarajiwa kurejea nchini anasema hatopigana pambano jingine lolote hivi karibuni hadi atakaporudiana na Smith.


“Nitarudi nyumbani siku mbili hizi, kuna vitu nakuja kuvifanya huko, lakini pia nitakuwa najifua hapo kisha kambi yangu itaahamia Marekani kidogo, nitafanya hivyo hadi Januari nitakaporudiana na Smith,” anasema.


Mwakinyo ameendelea kusalia kwenye nafasi ya 40 katika ubora wa ndondi duniani kwenye uzani wake, huku Smith pia akisalia kwenye nafasi ya sita na wote ni mabondia namba moja nchini mwao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad