Hatimaye Rais Kenyatta ampongeza mshindi wa kura za urais katika uchaguzi mkuu Kenya



RAIS Uhuru Kenyatta hatimaye amevunja kimya chake kuhusu matokeo ya kura za urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 yaliyomweka mbele naibu wake, Dkt William Ruto na hivyo kumaanisha kwamba ndiye atakayemrithi.

Katika hotuba yake kwa taifa Jumatatu jioni, Rais huyo anayeondoka amesema anaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Upeo wa kuidhinisha ushindi wa Dkt Ruto baada ya kesi iliyowasilishwa na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga wa Azimio la Umoja-One Kenya kutupwa na jopo la majaji saba.

Mahakama imesema Jumatatu mchana kwamba Ruto alichaguliwa kihalali.

“Nilipoapishwa kama rais, niliweka ahadi kuheshimu sheria. Leo Jumatatu Mahakama ya Upeo imeidhinisha matokeo ya urais kama yalivyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Ninaheshimu uamuzi wa korti,” amesema Rais Kenyatta.


Agosti 15, 2022, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Dkt Ruto kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha urais.

Raila hata hivyo alipinga ushindi huo, akitoa malalamiko kwamba kulikuwa na udanganyifu.

Rais Kenyatta alikuwa akimpigia debe Raila akisema ndiye kiongozi asiye na ubinafsi na tamaa ya kutaka kujitajirisha bali ana maono ya kutaka Wakenya wafurahie maendeleo na ustawi.


Wawili hao aidha wamekuwa wakishirikiana sako kwa bako tangu Machi 9, 2018, baada ya kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa kupitia maridhiano ya Handisheki.

Rais kwenye hotuba yake ambayo alionekana kutoridhishwa na maamuzi ya mahakama, amesema mipango ya mpito kumkaribisha Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya inaendelea.

“Kamati ya mpito imekuwa ikijiandaa tangu Agosti 10, 2022,” akasema.

“Kenya ni nchi inayoheshimu demokrasia, na ninahimiza watu waheshimu uamuzi wa korti. Ninashukuru Wakenya kwa kushiriki uchaguzi wa amani… Ninakushukuruni kwa kunipa fursa kuwahudumia na zaidi ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu,” amesema.



Akimpongeza mshindi, Rais Kenyatta hata hivyo hajamtaja Dkt Ruto kwa jina.

Rais mteule Dkt Ruto awali alikuwa amesisitiza kwamba serikali yake itaheshimu Bw Kenyatta kama Rais mstaafu. Dkt Ruto atakayeapishwa Jumanne, Septemba 13, 2022 majaliwa ameahidi kukamilisha miradi ya maendeleo waliyoanzisha pamoja katika serikali inayoondoka ya Jubilee.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad