Imeboreshwa Dakika 8 zilizopita
Raila Odinga alikuwa mstari wa mbele katika kampeni za kukomesha utawala wa chama kimoja katika miaka ya 1990, lakini hajawahi kufurahia matunda ya mapambano yake ya kuwa rais, baada ya kushindwa katika chaguzi kwa mara ya tano.
Katika hili, kisa chake kinafanana kwa namna fulani na kile cha babake, Jaramogi Oginga Odinga, makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, ambaye pia alishindwa kunyakua kiti cha urais licha ya mchango wake katika kampeni dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza.
Kipindi chake cha kwanza katika utumishi wa umma, mwaka 1974 Raila Odinga aliteuliwa kama meneja wa Shirika la kuangazia Viwango vya Bidhaa Kenya (KEBS) kabla ya kupandishwa cheo hadi Naibu Mkurugenzi mwaka 1978.
Miaka minne baadaye, Raila alizuiliwa na kushtakiwa kwa madai ya kuwa miongoni mwa waanzilishi wa mapinduzi ya 1982 yaliyojaribu kumpindua Rais wa zamani Daniel Arap Moi.
Baada ya kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani kwa miezi saba, Raila alinyimwa ruhusa ya kufungua kesi kwa miaka sita hadi 1988 wakati Moi alipoamuru kuachiliwa kwake.
Masaibu ya Raila hayakuishia hapo kwani alikamatwa tena mwaka huo huo na kuachiliwa 1989.
Waziri Mkuu huyo wa zamani pia alizuiliwa 1990 kwa kutetea demokrasia ya vyama vingi wakati ambapo nchi ilikuwa na chama kimoja.
Mwaka mmoja baadaye, Raila alitoroka nchini na kuelekea Norway ili kukwepa uwezekano wa kukamatwa.
Aliporejea mwaka wa 1992, Raila alijiunga na chama cha Forum for Restoration of Democracy (FORD-Kenya) na kuteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Kamati ya Madhumuni ya Jumla.
Wakati wa uchaguzi wa mwaka 1992, Raila alishinda kiti cha ubunge cha Langata kwa tikiti ya chama cha Ford-Kenya.
Baadaye alijiuzulu na kuunda chama cha National Development Party (NDP).
Mnamo 1997, hakufanikiwa katika jaribio lake la kwanza la urais kwa tiketi ya chama cha NDP na kuibuka wa tatu dhidi ya marehemu Mwai Kibaki na marehemu Daniel Arap Moi aliyekuwa mshindi.
Katika uchaguzi wa 2022, Raila Odinga alionekana kuwa na ushawishi mkubwa katika eneo ambalo lilikuwa halijawahi kumuunga mkono kwa wingi, Mlima Kenya.
Hii ilitokea baada ya Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta kuashiria wazi wazi na hata kuomba wafuasi wake kumuunga mkono Bw Odinga.
Mchango wa familia ya Uhuru katika safari ya Odinga kuwa Rais kuliwapa matumaini makubwa wafuasi wake kwamba hatimaye angechaguliwa na kuwa rais katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.
Je huu ndio mwisho wa Odinga kisiasa?
Chanzo cha picha, VARIOUS
Kiongozi wa Muungano wa Azimio nchini Kenya Raila Odinga
Maelezo ya picha, Kiongozi wa Muungano wa Azimio nchini Kenya Raila Odinga
Raila Odinga mwenye umri wa miaka 77, awali aliashiria kwamba iwapo angechaguliwa kuwa rais, basi ungekuwa mwisho wake madarakani.
Ukweli ni kwamba, umri wa Bw Odinga umeendelea kusonga na bila shaka halijakuwa jambo rahisi kwake kuendelea kusukuma gurudumu la siasa na umri wake.
Na baada ya Mahakama ya Juu Zaidi kutangaza kuwa William Ruto alichaguliwa kwa njia ya haki, Bwana Odinga kupata nafasi nyingine ya kujaribu kukata kiu yake ya kuwa rais, itakuwa ni miaka mitano ijayo atakapokuwa na umri wa miaka 82. Hiyo itakuwa mara yake ya sita kuwa mgombea wa urais iwapo atachukua hatua hiyo.
Pia haitakuwa kazi rahisi kumuondoa William Ruto kwenye kiti hicho ambaye kikatiba bado atakuwa anaweza kugombea kwa muhula mwingine wa miaka 5.
Ikumbukwe kwamba hata kama pengine Raila Odinga angeshinda urais katika uchaguzi huu ambapo William Ruto amethibitishwa kuwa mshindi na Mahakama ya Juu Zaidi, angeweka rekodi ya kuwa rais wa kwanza kushika madaraka akiwa na umri mkubwa zaidi.
Katika mahojiano na gazeti la eneo, kaka ya Raila Bwana Oburu Odinga, alisema kuwa "… ikitokea atashindwa kwenye uchaguzi, sasa tutamshauri aondoke na ajikite katika mambo mengine”.
Maelezo ya sauti, Hatima ya kisiasa ya Raila Odinga ni ipi?
Kikatiba, hakuma ukomo wa umri uliowekwa wa mtu kuacha kuwania urais.
Raila Odinga anatoka katika familia maarufu nchini Kenya na amekuwa kwenye ulingo wa kisiasa kwa miaka zaidi ya 40.
Alihudumu kama mbunge wa Lang'ata kwa miaka 20. Na kwa kipindi chote hicho, Bw Odinga amewania urais mara tano.
Akiwa na miaka 77, amejaribu kuwania urais kwa mara ya tano katika uchaguzi wa Agosti 9.
Katika nyadhifa ambazo amewahi kushika nchi Kenya, ya juu zaidi ilikuwa ya Waziri Mkuu 2008 alipoteuliwa katika serikali ya mseto.
Kwa mara ya tatu katika maisha yake, kiongozi huyo mkuu wa upinzani nchini Kenya amekuwa akipinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika Mahakama ya Juu Zaidi nchini humo. Na katika uchaguzi huu, ilikuwa ni jambo linalotarajiwa hasa baada ya kushindwa kwa kura kidogo.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa mawakili waliomuwakilisha hasa baada ya kuonekana kuwa Tume ya uchaguzi, safari hii ilijitahidi sana kuendesha uchaguzi uliokuwa wazi zaidi katika historia ya Kenya.
Ingawa kesi hiyo imetupiliwa mbali na Mahakama ya Juu Zaidi, bila shaka yoyote itatumiwa kama mfano katika chaguzi zijazo na kutumika kama fursa ya kuimarisha zaidi taasisi husika za uchaguzi.
Raila Odinga alishindwa na Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mara mbili na sasa William Ruto.
Nini kinafuata?
Raila Odinga
Chanzo cha picha, Reuters
Katika historia, Raila Odinga amekuwa akifahamika katika upiganiaji demokrasia nchini Kenya.
Amekuwa na historia ya kupigiwa mfano katika kupinga ufisadi na makundi ambayo kipaumbele chake ni maslahi binafsi.
Pia alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono marekebisho ya katiba mwaka 2010 na hata katika masuala ya kutetea haki za wanawake.
Kuna uwezekano mkubwa akaendeleza hili.
Aidha, kulingana na umri wake kuendelea kusonga mbele, ana chaguo la kuamua kutojihusisha na siasa, na badala yake kuanza kumshauri na kumfunza mmoja au wachache atakaowachagua mwenyewe kwa minajili ya kumrithi kisiasa.
Rais Uhuru Kenyatta amewahi kusema kwamba Raila Odinga ni mtu ‘’asiye na ubinafsi’’.
Wakati ambapo inaonekana kuwa mwisho wa safari yake ya kuwania urais kwa sasa baada ya Mahakama ya Juu Zaidi kuthibitisha ushindi wa William Ruto, Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja ndiye atakayekuwa kiongozi wa upinzani, jukumu ambalo ana uzoefu nalo sana.
Aidha, Bw Odinga anatambulika sana kimataifa.