TUANZIE wapi? Kuna mambo mawili mezani. Tuanzie na hili ambalo niliwahi kulisema zamani kwamba mchezaji kama Bernard Morrison anaweza kucheza katika kikosi chochote cha ukanda huu wa Afrika Mashariki, lakini katika timu yake ya Taifa Ghana haitwi.
Ni ukweli ulio wazi ambao unaonyesha tofauti kati ya soka la Afrika Magharibi kulinganisha na soka letu. Na hata Wacongo wanatuonyesha tofauti ya soka lao na letu. Kwamba hawana habari kama kuna mtu anatetema huku Tanzania.
Mchezaji kama Fiston Mayele anaweza kuanza katika kikosi cha Uganda, Kenya, Tanzania, Malawi na hata Zambia lakini hajaitwa katika kikosi cha DR Congo na wala sidhani kama anafikiriwa kuitwa. Ukitazama safu ya washambuliaji wa DR Congo waliopo nje ya nchi yao ni vigumu kumuita Mayele.
Tazama mpira anaoucheza Yannick Bangala. Naye hajaitwa. Ni mchezaji ambaye Taifa Stars anaanza kila mechi na anakuwa staa mkubwa. Yeye na Djuma Shaaban waliwahi kuitwa wakati wakiwa nchini, lakini sasa hawajaitwa tena.
Kulikuwa na uongo umeanza kusambaa kuhusu staa wa Simba, Pape Sakho kuitwa katika kikosi cha taifa cha Senegal. Kilikuwa kichekesho cha hali ya juu. Uwaache mastaa kadhaa wanaocheza kiwango cha juu Ulaya na kumchukua staa wa Simba? Haiwezekani.
Kilicho wazi ni kwamba hata kutoitwa kwao sio mjadala kwao. Kwanini sio mjadala? Kwa sababu wachezaji walioitwa kucheza katika nafasi zao wana ufundi mkubwa kama wao. Na sio ajabu ambacho kinawabeba zaidi ni kwamba wanacheza katika ligi kubwa zaidi kuliko ya Tanzania.
Inawezekana ambacho kwa kiasi kikubwa kimemsaidia Inonga ni ukweli kwamba labda katika eneo lake hakuna walinzi wa kutosha katika ligi yao au nje. Labda Inonga alishatengeneza wasifu mkubwa hapo nyuma na katika nafasi yake hakuna wachezaji wengi nje.
Lakini labda mchezaji mwingine wa Simba ambaye angeweza kuitwa katika timu kubwa ya taifa la Afrika ni Aishi Manula kama asingekuwa Mtanzania. Kuna tatizo la makipa kwa mataifa makubwa. Sio wengi wanaocheza Ulaya na ndio maana Ghana inaweza kumuita kipa anayecheza Afrika Kusini. Na ndio maana haishangazi kuona Djigui Diarra anaitwa Mali.
Hii ina maana mbili. Haya mambo hayaji kwa bahati mbaya. DR Congo imekuwa ikizalisha wachezaji wetu. Kuna wale ambao wanazalishwa ndani na kuna wale ambao wamezaliwa nje. Hata hivyo kwa wale wanaozalishwa ndani wapo wachezaji wa aina mbili.
Kuna wale ambao wanakwenda nje halafu kuna wanaobaki ndani. Kwa mfano, Yanga walimchukua Mayele akiwa anacheza ndani. Unaweza kumuona Mayele ni hatari kiasi gani, lakini kuna kina Mayele wengi ndani na nje. Sio wanaocheza Ulaya, bali wapo wanaocheza Afrika.
Ni kama Cesor Manzoki ambaye alikaribia kutua Simba. Huyu naye ni zao la ndani ya DR Congo na baadaye akajikuta anaangukia nchini Uganda. Baada ya kupiga hizi hesabu ndipo unapomgeukia mchezaji anayeitwa Mbwana Samatta.
Kwamba DR Congo yenye vipaji lukuki kama hivi vya kina Mayele bado walimtegemea kijana mmoja mdogo kutoka Mbagala, Tanzania kwa ajili ya kufunga mabao katika timu yao kubwa zaidi kwa sasa - TP Mazembe. Hapo ndipo unapojua Samatta alipambana kiasi gani kutamba DR Congo.
Wakati Samatta anacheza DR Congo kulikuwa na washambuliaji mbalimbali katika timu za DR Congo, lakini yeye alionekana kuwa bora kuliko wao. Tangu alipoingia DR Congo hadi alipoondoka hakukuwa na mshambuliaji wa DR Congo aliyewahi kumuondoa katika nafasi yake.
Wakati anacheza kule hawa kina Mayele na Manzoki wote walikuwa wanacheza ligi ya DR Congo lakini Moise Katumbi hakuwahi kushawishika kumuondoa Samatta na kununua mastaa wengine washambuliaji ndani ya DR Congo.
Wakati mwingine watu tunamchukulia poa zaidi Samatta na ni kitu ambacho huwa kinanisikitisha. Watu wengi wanadhani lilikuwa suala la kawaida tu kwa Samatta kwenda DR Congo na kucheza. Halikuwa suala rahisi.
Ni sawa unapomuona Muargentina au staa kutoka Ecuador anakwenda kucheza soka la kulipwa Brazil katika klabu za Flamingo, Vasco da Gama, Palmeras au nyinginezo. Haiwi rahisi. Ni lazima awe na kitu kikubwa kuliko Wabrazil wenyewe. Kuna Wabrazil wangapi ambao wangeweza kucheza katika nafasi yake? Na zaidi ya yote baada ya mastaa wengi kutamba ndani ya DR Congo wana nafasi kubwa ya kucheza Ulaya hasa katika nchi za Ubelgiji na Ufaransa ambazo ni baba koloni kwa DR Congo. Hata hivyo unachokiona ndio hali halisi. Wazungu walimchukua Samatta na kuwaacha Wacongo wengi ambao wameendelea kucheza nyumbani.
Haya mambo mawili Watanzania hawayazingatii kwa umakini. Jambo la Samatta kutesa DR Congo lakini pia kuondokea DR Congo kwenda Ulaya. Wanadhani ni kitu cha kawaida tu. Wanapomuona Mayele yuko hapa na Samatta anacheza Ulaya hawapimi ubora wa Samatta. Tukiachana na hilo, kuitwa kwa Inonga pekee ni funzo. Nafahamu kwamba Aziz Ki ameitwa kwao Burkina Faso na pia Yacouba Sogne alikuwa akiitwa wakati fiti, lakini taifa lao sio kubwa sana kisoka kulinganisha na mataifa kama Nigeria, Ghana, Cameroon, Ivory Coast na mengineyo.
Lazima tujikumbushe pengo kubwa lililopo baina yao na sisi. Wakati mwingine huwa tunawapa madeni makubwa wachezaji wa timu ya taifa pindi wanapocheza na mataifa haya au Wacongo tukiamini kwamba tunaweza kushinda kiurahisi. Linapokuja suala la timu ya taifa tunasahau kwamba hata Wacongo wanaweza kutengeneza kikosi cha kwanza kilichopo hapahapa nchini na wakashinda mechi dhidi ya Taifa Stars. Tunapouona ubovu wa kikosi cha Taifa Stars huwa tunasahau mambo haya muhimu.
Mwanaspoti