Huyo Chama Kazaliwa Upyaa Simba




KIKOSI cha Simba baada ya kurejea nchini kikitokea Sudan kilipoenda kwenye michuano maalumu iliyoandaliwa na Klabu ya Al Hilal, lakini gumzo likiwa ni kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama ambaye amezaliwa upya na Kocha Zoran Maki kushindwa kujizuia.

Zoran aliyekuwa akidaiwa hakuwa akimkubali kiungo huyo amekiri Chama ni habari nyingine kwani ni mchezaji wa daraja la juu na anaamini akiendelea na moto aliouonyesha hadi sasa ataipaisha Simba kwenye Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika inayosimamiwa na CAF.

Katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara, Chama amehusika kwenye mabao manne kati ya matano ambayo timu hiyo imeyavuna, akisisti matatu na kufunga moja, huku akiwa Sudan Mwamba huyo wa Lusaka aliupiga mwingi na kuwa gumzo kwa nyota wa timu hiyo iliyopoteza juzi kwa bao 1-0 kwa Al Hilal.

Ubora wa Chama ulionekana kwenye mechi dhidi ya Asante Kotoka ya Ghana ambapo Simba ilishinda 4-2 kabla ya juzi tena kufanya kazi kubwa, licha ya timu kupoteza na kiungo huyo alisema kurejea kwenye ubora wake kumetokana na maandalizi mzuri kupitia nchini Misri na pia kupona kwa majeraha yaliyomsumbua tangu aliporejea kutoka RS Berkane.


Chama aliliambia Mwanaspotia baada ya kurudi Simba msimu uliopita hakucheza kama alivyotarajia na sababu ilikuwa ni majeraha ila baada ya kupata muda wa kupumzika na matibabu sasa yupo fiti.

“Msimu huu Simba inahitaji kufanya vizuri na kushinda mataji yote hayo hayatawezekana bila ya wachezaji kuwa katika viwango bora ili kupigania malengo yetu kwani si kazi rahisi kutokana na ushindani uliokuwepo,” alisema Chama na kuongeza;

“Nilichoonyesha mechi za nyuma yote yameshapita, nimejipanga kufanya vingine bora ili timu iweze kushinda kila mchezo uliokuwa mbele yetu na yote hayo yatawezekana kutokana na ushirikiano wa wachezaji wenzangu.


“Ukiangalia ubora wa wachezaji tuliokuwepo msimu uliopita na wapya walioongezeka kuna kitu kitaongezeka katika ushindani na kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita katika mashindano yote.”

Kocha wa kikosi hicho ambacho kesho kitashuka tena uwanja kuvaana na AS Arta Solar 7 ya Djibouti katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kuivaa KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara Alhamisi ijayo, Zoran Maki alisema Chama ni mchezaji wa daraja la juu.

Zoran alisema Chama amekuwa na ubora timu inaposhambulia, mtulivu akiwa na mpira anaweza kupiga pasi ya mwisho ya uhakika.

Alisema Chama anaweza kutengeneza nafasi za kufunga na amefanya hivyo katika ligi hadi michezo ya kirafiki na uzuri anafunga mwenyewe muda mwingine kulingana na shambulizi lilivyo.


“Nahitaji kuona Chama anafanya hivi si katika mashindano ya ndani hadi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, akifanya hivyo ni miongoni mwa silaha ya kufanya vuzuri katika michezo yetu,” alisema Zoran.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad