Jela Mwaka Mmoja kwa Kutoa Taarifa za uongo Kujipatia Nida



Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu jijini Dar es Salaam, imemhukumu raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Said Issa(42) kulipa faini ya Sh 1.1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja na mwezi mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo na kisha kujipatia kitambulisho cha Taifa (Nida), kinyume cha sheria.

Issa ambaye ni mkazi wa Magomeni, amehukumiwa kulipa faini hiyo, leo Jumatatu Septemba 12, 2022 baada ya kukiri mashtaka yake.

Akitoa Hukumu, Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

"Katika shtaka la kwanza, ambalo ni kuishi nchini bila kuwa na kibali, Mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh 500,000 na ukishindwa utatumikia kifungo cha miezi sita jela," amesema Hakimu Kyaruzi na kuongeza


"Katika shtaka la pili, ambalo ni kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Uhamiaji kuwa wewe ni raia wa Tanzania na Kisha kujipatia kitambulisho cha Taifa, Mahakama hiii inakuhukumu kulipa faini ya Sh 600,000 au kwenda jela miezi saba" amesema Hakimu.

Hata hivyo, Hakimu Kyaruzi amesema adhabu hiyo inakwenda kwa pamoja.

Mshtakiwa ameshindwa kulipa faini na hivyo atatumikia kifungo hicho.


Awali, Wakili kutoka Uhamiji, Godfrey Ngwijo, aliomba Mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria dhidi ya mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, mshtakiwa ameomba Mahakama imsamehe na impunguzie adhabu kwa kuwa ndio kosa lake la kwanza.

Katika kesi ya msingi, mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 6, 2022 akiwa ni raia wa Kidemokrasia ya Congo alikutwa eneo la Magomeni akiishi nchini bila kibali.

Shtaka la pili, siku hiyo akiwa ofisi ya uhamiaji wilaya ya Kinondoni, aliwapotosha maofisa wa uhamiaji kuwa ni raia wa Tanzania na kisha kujipatia kitambulisho cha Taifa (Nida) wakati akijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na yeye sio raia wa Tanzania.


Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake, alikiri na ndipo upande wa mashtaka walipomsomea hoja za awali na Kisha Mahakama kumtia hatiani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad