KITU ambacho unaweza usiwe na uhakika nacho ni ukweli kwamba siku kadhaa zijazo Yanga watacheza moja kati ya mechi ngumu katika historia yao miaka ya karibuni dhidi ya Al Hilal na nahodha wao, Bakar Mwamnyeto ataishia katika benchi. Imekuwa kitu cha kawaida kwa siku za karibuni.
Lakini zaidi ni kwamba Mwamnyeto pia kwa sasa hayupo katika kikosi cha timu ya taifa pale Libya. Inaweza kuwa ni mara ya kwanza baada ya miaka mingi kupita kwa Mwamnyeto kuachwa katika kikosi cha timu ya taifa. Mara zote amekuwa beki tegemeo kikosini. Na labda huenda sio nahodha wa timu ya taifa kwa sababu ya uwepo wa Mbwana Samatta.
Nini kinamtokea Mwamnyeto? Sifahamu. Ninachojua anapitia wakati mgumu. Hachezi vizuri. Ana makosa mengi. Ukabaji wake pia ni duni. Haishangazi kuona katika kikosi cha Kocha Nasreddine Nabi kwa sasa analazimika kumrudisha Yannick Bangala kucheza sambamba na Dickson Job katika nafasi ya beki ya kati.
Hivi ni namna ambavyo maisha yamekwenda kasi kwa Mwamnyeto. Kutoka kugombaniwa na Simba na Yanga wakati ule akiwa bidhaa adimu sokoni. Halafu Yanga ikalipa mamilioni kupata saini yake. Halafu akapewa kitambaa cha unahodha Yanga. Lakini leo anakaa benchi pale Yanga na hajaitwa timu ya taifa.
Walio karibu naye wanadai ana matatizo binafsi, lakini ukweli mchungu katika soka mashabiki huwa hawana muda wa kusikiliza hadithi ya matatizo binafsi ya nje ya uwanja. Wanachojali ni kiwango chako uwanjani. Hivi ndivyo namna ambavyo mashabiki walivyo wabinafsi. Hauwezi kuwalaumu.
Mbaya zaidi inapotokea wakati unacheza Simba au Yanga. Presha ni kubwa. Kila mechi ni fainali. Unaweza kujificha katika kivuli kama unacheza Namungo, Geita Gold au Mbeya City lakini sio Simba na Yanga. Presha ni tofauti na ni ya aina yake.
Kuna rafiki yangu anaitwa Lucas Kikoti pale Namungo. Ni fundi hasa wa mpira lakini ana msimu wa pili sasa anachocheza uwanjani hakieleweki kabisa. Hakuna anayemzungumzia kwa vile hachezi Simba wala Yanga. Hii ndio faida ya kucheza katika timu ndogo ambazo hazina mashabiki wengi na wala vyombo vya habari haviwafuatilii.
Zinapotokea nyakati kama hizi kwa Mwamnyeto jibu huwa linatoka kwa mchezaji mwenyewe. Inabidi aendelee kukaza kweli kweli. Yeye sio mchezaji wa kwanza kuwa katika hali hii. Hakuna mchezaji ambaye hapiitii hali hii. Hata Lionel Messi na Cristiano Ronaldo nao hujikuta katika hali hii.
Mchezaji mkubwa ni yule ambaye anajibu mapigo baada ya hali hii kumtokea. Unajaribu kuimarika zaidi kwa sababu ya ukweli soka ni kazi yako. Lakini hapohapo usingependa kuifanya kazi hii katika timu ndogo baada ya kuachwa na timu kubwa. Ukweliulkuko hivi, ukiachwa na Yanga basi Simba na Azam haziwezi kukufuata. Utaangukia Geita Gold au Namungo. Maisha yatakuwa tofauti.
Lakini hapahapa tunaweza kujikumbusha endapo kiwango cha Mwamnyeto kitaendelea kudumaa basi kuna uwezekano mkubwa Yanga wakaenda sokoni kusaka beki wa kati wa kigeni. Hii ina maana idadi ya wazawa wanaoanza katika vikosi vya timu kubwa hasa Simba na Yangaa ikapungua kwa mara nyingine.
Mastaa wanaoanza katika vikosi hivi huwa wanahesabika kwa vidole. Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Shomari Kibwana, Dickson Job, Aishi Manula, Mzamiru Yassin, Fei Toto na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’. John Bocco yupo maji ya jioni. Hata asipoanza huwa hatuna lawama naye.
Mwamnyeto akiharibu Yanga usidhani klabu hiyo italeta beki wa ndani. Yanga ina hela. Italeta beki wa kigeni na kumrudisha Bangala katika nafasi yake ya kiungo. Maisha yataendelea. Hata pale Simba, Tshabalala na Kapombe wakifika ukingoni nadhani Simba watasafiri kwenda nje kuleta mchezaji wa kigeni.
Jambo hili halina afya kwa timu ya taifa. Kwa nini? Wazawa wanaopata nafasi katika vikosi vya Simba, Yanga na Azam ni rahisi kuimarika zaidi kuliko wazawa wanaocheza klabu nyingine kwa sababu mara nyingi wanajikuta wanacheza katika michuano ya kimataifa.
Wanaanzia katika siku zao maalumu za ufunguzi wa msimu kama vile Simba Day na Wiki ya Wananchi. Jaribu tu kufikiri kwamba sasa hivi Azam ilikuwa Zambia ikicheza mechi za kirafiki za kimataifa lakini majuzi tu Simba ilikuwa Sudan ikifanya hivyo.
Mwamnyeto anapoondoka katika kikosi cha kwanza athari zake zinasambaa hadi Stars, ingawa mashabiki wengine hawawezi kuliona jambo hilo kwa urahisi. Kama ingekuwa tuna wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi tungeweza kukaa kimya lakini hadi sasa mastaa wanaoijaza Stars wanatoka ndani ya ligi yetu.
Mwamnyeto apambane arudi katika hali yake. Wakati mwingine huwa inamtokea mchezaji katika kipindi kifupi, lakini wakati mwingine uwezo wa kujiamini unaweza usirudi tena. Hofu yangu iko hapo. Mchezaji anapoondokewa uwezo wa kujiamini anajikuta anafanya makosa zaidi na zaidi na anapoteza kila kitu.
Pale Manchester United kuna beki anaitwa Harry Maguire. Alikuwa hodari akiwa Hull City kisha Leicester City halafu Man United wakamnunua kwa pesa nyingi. Alianza vizuri lakini ghafla akawa na makosa mengi. Tulidhani yangefutika kwa sababu alicheza vizuri fainali za Kombe la Dunia la Russia siku zinaenda tunamsubiri Maguire tuliyemjua hatumuoni. Mwamnyeto asije akawa Maguire wetu. Hivi tunavyozungumza Maguire amepoteza nafasi yake ya kudumu kikosini na hapana shaka anaweza kupoteza unahodha wake.