Juma Mgunda arejesha heshima Simba SC



AKIWA ameiongoza kwenye mechi mbili tu, mabosi wa Simba wameonekana kufurahishwa na mwanzo mzuri wa Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda, wakisema ameleta hali ya upambanaji ndani ya kikosi chao, imeelezwa.

Simba itashuka dimbani kesho kuwakaribisha Nyasa Big Bullets, kutoka Malawi katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema ujio wa kocha huyo umebadilisha hali za wachezaji ambayo haikuwepo kabla ya kocha huyo kuwasili ambapo sasa kila mmoja anapambana na kujituma tofauti na ilivyokuwa katika mechi tatu za mwanzo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ahmed alisema, hata kwenye mechi dhidi ya Prisons, kama isingekuwa wachezaji kujituma na kupambana, bao lililopatikana dakika tano kabla ya mechi huenda lisingefungwa.

"Kwa kweli kocha Mgunda ameongeza ari kubwa ya kupambana, wachezaji sasa wanajituma mno, wanacheza 'jihad' kitu ambacho kilikosekana muda mrefu ndani ya Simba. Ukitazama mechi ya Prisons utaelewa kile ninachokisema. Katika mechi zetu tatu za mwanzo ulikuwa unaona, mbili tulishinda lakini hawakupambana, timu ilicheza kama bonanza hivi, walikuwa wanacheza kivivu, lakini angalia baada ya kuingia yeye, dhidi ya Nyasa Big Bullets walivyopambana, tazama dhidi ya Prisons. Siku ile dhidi ya Prisons kama siyo kupambana tusingepata bao, ufundi, mbinu zilikwisha.

Katika mechi hiyo hapo unahitaji mikimbio zaidi ya wachezaji, na ndiyo maana unaona hata goli limefungwa na Mkude (Jonas) ambaye ni kiungo mkabaji, na si mfungaji wa mara kwa mara, lakini kwa sababu ya kupambana na wenzake, wakafanikiwa," alisema Ahmed.

Ofisa huyo aliongeza Mgunda aliwakabidhi wachezaji jukumu la kupambana kwa ajili ya nembo ya klabu, wanachama na mashabiki, pamoja na kupambania yeye kocha.

"Aliwaambia nyinyi wachezaji ndiyo wa kuwaonyesha watu kama mimi ni kocha kweli au wa kubabaisha. Simba ndiyo timu iliyosajili wachezaji wazuri zaidi msimu huu, lakini kilichokosena ni upambanaji, lakini sasa inaanza kurejea kidogo, baada ya muda mfupi kutakuwa na balaa kubwa hapa nchini," alitamba Ahmed.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad