Kenya: Rais Kenyatta ‘Ampotezea’ Mteule Ruto

 


Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameshindwa kumpongeza mrithi wake mpya William Ruto siku chache baada ya Mahakama ya Juu ya Kenya kuthibitisha tena matokeo ya kura.


Ruto amesema, Kiongozi huyo anayemaliza muda wake huenda hajaona vyema kumpongeza baada ya kumshinda mgombea wake mkuu, Raila Odinga.


Amesema, “Nimeshinda uchaguzi huo ndio muhimu ila kwa bahati mbaya, Rais Kenyatta hajaona inafaa kunipongeza lakini nadhani ni sawa labda amekatishwa tamaa, au hana furaha kwamba nilimshinda mgombea wake lakini pia hilo ni asili ya siasa.”


Kuhusu kiini cha uchaguzi wa amani na jinsi ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi uliopita, Ruto amesema Wakenya wameendelea kukomaa kisiasa na demokrasia yao inaimarika.


“Ninazungumzia moyo wa ukomavu wa demokrasia ya nchi yetu, hakuna mwananchi wala kiongozi anayetaka nchi yao ijulikane kwa vurugu, tunaenda kwenye uchaguzi na kuchagua viongozi wetu na siku inayofuata tunarejea kazini,” amebainisha Ruto.


Hata hivyo, Ruto amedokeza kwamba alikuwa na mazungumzo ya simu na Kenyatta na Odinga na alisisitiza kwamba atafanya kazi na kila mtu hata kutoka upinzani na atakuwa rais wa Wakenya wote.


Rais, Uhuru Kenyatta alikuwa aliahidi kuwa kutakuwa na mabadiliko ya mamlaka ingawa alishikilia msimamo wake kuwa kiongozi wake atakuwa ni Raila Odinga daima.


Aidha, Ruto amekuwa Naibu Rais chini ya Kenyatta tangu mwaka 2013, akimuunga mkono katika chaguzi mbili kwa ahadi kwamba angeungwa mkono pia katika uchaguzi wa mwaka huu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad