KESI YA MAUAJI- Mkemia adai huenda mwili ulichomwa kabla kufukiwa



MKEMIA Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kaijunga Brassy ameiambia mahakama mabaki ya mwili wa marehemu Farihani Maluni, ikiwamo mifupa, hayakuonyesha majibu ya vinasaba kwa sababu ulikuwa na udhahiri mdogo.

Pia amedai mwili huo ambao ulifukiwa mbele ya  nyumba iliyoko Ilala Sharif Shamba inawezekana ulichomwa moto kabla haujazikwa au ardhi aliyozikwa ilikuwa na chumvi, hivyo seli hazikuwa na muunganiko.

Brassy alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya Hemed Ally anayetuhumiwa kumuua Maluni na kumfukia.

Alidai kuwa vielelezo alivyovifanyia uchunguzi huo ni mifupa miwili ya paja, nguo ya ndani ya marehemu, plasta, mifupa ya kwenye kiuno, kamba na nguo yenye vifungo, meno, fuvu la nyuma la kichwa, mkanda, upindo wa suruali na kola ya shati.

Alidai barua ya kufanya uchunguzi wa vitu hivyo pia ilimtaka afanye uchunguzi wa vinasaba vya Abisalum Maluni ambaye ni baba wa marehemu, Faisal na Fahadi (watoto wa marehemu), ambapo aliwachukua mipanyuso mitatu ya kinywa.


Alidai kuwa uchunguzi huo wa vinasaba ulikuwa na lengo la kufananisha mabaki ya marehemu na ndugu hao ili walinganishe vinasaba vyao kama Farihani ni ndugu yao.

Alidai vielelezo hivyo alivipa namba za usajili 115/2015 na baadaye alivihifadhi na akaja kuvifanyia kazi Julai 27/2018 na alibaini kuwa vielelezo namba moja hadi nane havikutoa majibu ya vinasaba.

Hata hivyo, kielelezo namba tisa - baba na watoto wa marehemu vilitoa majibu ya chembe halisi za urithi, katika kulinganisha vilifanana vinasaba vya watoto na baba wa marehemu Farihani.

"Kielelezo namba moja hadi nane yakiwamo mabaki ya mwili wa Maluni havikutoa majibu kwa sababu havikuwa na udhahiri, inawezekana huo mwili ulichomwa moto kabla haujazikwa au ardhi aliyozikwa ilikuwa na chumvi, hivyo seli hazikuwa na muunganiko," alidai.

Awali Brassy alidai Februari 12, 2015 akiwa ofisini, alipokea vielelezo na barua kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam wakiomba uchunguzi wa vielelezo tisa.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Jumatatu saa tatu asubuhi. Inadaiwa Juni mwaka 2014, Hemed Ally alimuua Farihani Maluni eneo la Sharif Shamba ndani ya Wilaya ya Ilala,  Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad