ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Mali za Shirika la Reli (RAHCO), Benhardard Tito, amepatikana na kesi ya kujibu katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Aidha, Mahakama hiyo imewaachia Mwanasheria wa RAHCO, Emmanuel Massawe na mfanyabiashara ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma, baada ya kutokuwakuta na kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi Rhoda Ngimilanga, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi tisa wa upande wa Jamhuri na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani dhidi ya washtakiwa hao.
Ngimilanga alisema ushahidi uliotolewa haukumgusa mshtakiwa wa pili (Massawe) na Mwinyijuma, kwa hiyo mahakama haijawakuta na kesi ya kujibu, hivyo Tito pekee ndiye anatakiwa kujitetea kwa sababu amepatikana na kesi ya kujibu.
Kutokana na kukutwa na kesi ya kujibu, Tito anatarajia kuanza kujitetea Oktoba 13, mwaka huu.
Awali, Wakili wa Serikali, Iman Nitume, aliieleza mahakama kuwa kesi imeletwa kwa ajili ya uamuzi na wako tayari kwa uamuzi huo.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwamo uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kuisababishia RAHCO hasara ya Dola za Marekani 527,540.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa, walikula njama kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Ilidaiwa kuwa Februari 27, 2015 katika ofisi za RAHCO zilizoko, Ilala jijini Dar es Salaam, Tito alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya RAHCO.
Ilidaiwa kuwa Tito na Massawe, Machi 12, 2015 katika ofisi za RAHCO, wakiwa katika nyadhifa zao, walitia saini barua ya kuihalalisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi huo.
Katika shtaka lingine, ilidaiwa kuwa Tito na Massawe, Machi 12 na Mei 20, 2015 wilayani Ilala walishindwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini na RAHCO.
Tito na Massawe wanadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi za RAHCO, kwa kutumia madaraka yao vibaya, walitia saini mkataba wa kutoa huduma za ushauri na kampuni ya Afrika Kusini bila ridhaa ya Bodi ya Zabuni ya RAHCO.
Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kuwasilisha mkataba walioingia na Kampuni ya Afrika Kusini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.