Kijana Ajinyonga Kituo cha Polisi Moshi, Familia yang'aka



Moshi. Nicholaus Mushi (27) amefariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia tambara la dekio, akiwa mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Taarifa zilizotolewa na ndugu wa marehemu, zanadai kabla ya kujinyonga, alijaribu kujiua kwa kujikata kwenye koromeo na wembe akiwa mahabusu.

Hata hivyo, askari walimuwahi na kumpeleka hospitali kwa matibabu na aliporudishwa ndipo usiku alijinyonga.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 14, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.


Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mwenyekiti wa Mtaa wa Njoro Sokoni, Rabia Lema alikokuwa akiishi marehemu, amesema marehemu alikamatwa Septemba 10, 2022 na kufikishwa kituoni hapo ambapo alikuwa akituhumiwa kuiba simu ya mkononi na kompyuta mpakato.

Lema amesema alipigiwa simu usiku wa kuamkia Septemba 13,2022 na askari akitakiwa kufika kituo cha Polisi Kati mjini Moshi akiambiwa kuna tatizo la mahabusu kujinyonga na katika maelezo yake aliandika anaishi Njoro Sokoni.

"Ilikuwa saa 9:43 usiku, tulipopigiwa simu, tulienda kituoni na baadhi ya wajumbe wa serikaki ya mtaa na polisi jamii, tulipelekwa chumba cha mahabusu, tulikuta wengine wamelala, tukaingizwa chooni, tukakuta kweli mtu ananing'inia amejinyonga kwa dekio na baada ya kumuangalia nilimtambua," amesema


Amesema, "na nilipofuatilia nikaambiwa alikuwa amepelekwa Polisi akituhumiwa kwa wizi wa simu na kompyuta mpakato, nilikuwa sifahamu ndugu zake na nililazimika kuomba vijana waliokuwa nae mtaani hapa wasaidie ili ndugu wapatikane. Nitoe pole kwa familia, na niwasihi vijana waachane na tabia ya udokozi watafute kazi halali za kuwaingizia kipato".

Kwa upande wake, Dada wa marehemu, Angella Mushi amesema kifo cha ndugu yake kimewaacha na maswali mengi kwa kuwa maelezo waliyoyapata polisi kuhusiana na kifo hicho yana utata.

"Mtu yuko mahabusu, tunaambiwa amejinyonga na dekio, tunajiuliza hilo dekio mpaka achane apate kamba ya kujitundika, lilikuwa ngumu kiasi gani? Lakini pia tunaambiwa kabla ya kujinyonga alijikata kwenye koromeo na wembe na wakampeleka hospitali, sasa swali la kujiuluza ni kwamba aliwezaje kuingia mahabusu akiwa na wembe? alihoji dada wa marehemu.

"Lakini pia tunaambiwa alijaribu kujiua kwa kujikata na kiwembe, sasa tunajiuliza kama mtu alishajaribu tukio la kujiua walimrudishaje kwenye chumba chenye mazingira hatarishi? bado familia tuna maswali, lakini tunajua hatuwezi kushindana na serikali, ila tukio kama hili wakati mwingine linahitaji umakini," amesema


Awali, bibi wa marehemu, Agness Mahenge, Mkazi wa Kata ya Miembeni, Manispaa ya Moshi, amesema yeye alipata taarifa za kifo cha mjukuu wake Septemba 13, 2022 saa 7 mchana kutoka kwa mwanae anayefanya kazi stendi kuu ya mabasi mjini Moshi.

"Nilipigiwa simu na mwanangu ambaye ni mama mdogo wa marehemu, akinipa taarifa za kifo cha mjukuu wangu, alinieleza taarifa alizopewa ni kwamba marehemu alijikata kwenye koromeo na wembe ambapo alipelekwa hospitali ya Mawenzi kutibiwa na kurudishwa mahabusu," amesema

"Wanasema baada ya kurudishwa kituoni, aliingizwa chumba cha mahabusu na saa 8:00 usiku alijinyonga kwa tambara la dekio.

"Wanadai walitutafuta ndugu na hawakutupata kwa kuwa marehemu katika maelezo yake polisi aliandika hana ndugu na anaishi Njoro sokoni na ndiyo maana waliita uongozi wa mtaa huo kufika kuutambua mwili," amesema

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad