Dar es Salaam. Baada ya kesi ya waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18 dhidi ya chama chao hicho cha zamani kukwama kusikilizwa, Agosti 26, 2022 sasa kesi hiyo inatarajiwa kuanza kuunguru leo Ijumaa, Septemba 30, 2022.
Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam, wakipinga kufukuzwa uanachama kwa kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).
Kesi hiyo iliyofunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu, imepangwa kusikilizwa leo Ijumaa na Jaji Cyprian Mkeha, ambapo wakati wa usikilizwaji huo Mdee na wenzake saba watalazimika kufika mahakamani kwa ajili ya kuhojiwa na mawakili wa Chadema kuhusiana na madai yao.
Mdee na wenzake hao saba wanalazimika kufika mahakamani kuhojiwa baada ya mawakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala kuiomba mahakama iamuru wawepo siku ya usikilizwaji ili wapate nafasi ya kuwafanyia madodoso, na mahakama ikaridhia ombi hilo.
bb
Mbali na Mdee wengine walioitwa ni Nusrati Hanje, Ester Matiko, Ester Bulaya, Jesca Kishoa, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga na Cecila Pareso.
Hata hivyo, mawakili wa kina Mdee pia walishaieleza mahakama nia yao ya kutaka kuwahoji baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema na watu wengine ambao viapo vyao kinzani vimewasilishwa mahakamani katika kujibu hoja za kina Mdee.
Hiyo inaonesha wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kutaukuwa na mchuano mkali wa hoja na maswali na majibu kutoka kwa mawakili wa pande zote dhidi ya wadai na wadaiwa.
Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya Wadhamini, wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama niaba ya Bunge la Tanzania; na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, Mdee na wenzakeo wanaowakilishwa na mawakili Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu wanapinga uamuzi uliotolewa na Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022.
Wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza kisha itoe amri tatu.
Amri hizo ni ya kutengua mchakato na uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama (certiorari order), kukilazimisha Chadema kutimiza wajibu wake kisheria (mandamus), yaani kuwapa haki ya kusikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.
Uamuzi huo wa Baraza Kuu ulitokana na rufaa walizozikata kina Mdee kupinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu, Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, bila ridhaa ya chama.
Kina Mdee pamoja na mambo mengine wanadai kuwa mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama haukuzingatia matakwa ya kisheria na misingi ya haki, wakidai kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa, kuanzia Kamati Kuu mpaka Baraza Kuu walikokata rufaa.
Pia wanadai kuwa walifukuzwa kwa makosa yasiyo na maana na yasiyoweza kuthibitika, kuwa walikula njama kujiteua mwenyewe na kuapa kuwa wabunge wa viti maalum.
Katika viapo vyao wanadai kuwa mara tu baada ya kula kiapo, Novemba 24,2020, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amtaja yeye na wenzaek kama wasaliti, huku wakiitwa Covid-19 na kwamba walishahukumiwa na viongozi wa chama hicho hata kabla ya vikao vya vyombo husika.