KUONYESHA hana utani na kibarua ambacho amepewa na Simba, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda alianza kutekeleza majukumu yake kikosini humo kwa kuitisha vikao viwili vizito vilivyohusisha baadhi ya viongozi waliosafiri na timu, benchi la ufundi na wachezaji wote.
Mgunda aliweka kikao hicho mara baada ya timu hiyo kuwasili nchini Malawi ambapo Simba watacheza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya wenyeji wao Nyasa Big Bullets.
Chanzo chetu kutoka Malawi kimeliambia Championi Jumamosi kwamba, mara baada tu ya juzi Alhamisi Simba kuwasili nchini Malawi, kocha na baadhi ya viongozi wa Simba, waliitisha kikao cha pamoja wakiwataka wachezaji kukubaliana na hali ya mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi, huku wakiwataka kutokatishwa tamaa wala kuwazia mabadiliko hayo zaidi ya kujikita kwenye mchezo.
“Uongozi umetumia fursa ya kumtambulisha Mgunda kwa wachezaji, huku ukiwataka kutofikiria wala kujitoa mchezoni kutokana na mabadiliko hayo na badala yake, wamewaomba kuuachia uongozi mambo yote ya kiutendaji na wao waendelee kuwapa ushirikiano makocha, hadi pale watakaposikia taarifa mpya za mabadiliko sahihi.
“Mbali na kikao hicho pia Kocha Mgunda na Selemani Matola nao kwa pamoja walipata fursa ya kufanya kikao chao binafsi na wachezaji, na kuwaomba wasiwazie kuwepo na mabadiliko yoyote ya kikosi kwani hawatafanya jambo jipya zaidi ya kuendelea na misingi iliyopo kufutana na mahitaji ya mchezo.
“Kocha amesema kila mmoja anatakiwa kupambana ili timu upate ushindi, kwani wao wapo kwa ajili ya kuwakumbusha mambo muhimu na siyo kuvuruga utaratibu wa awali, hivyo kawataka kutokuwa na hofu yoyote zaidi ya kuwazia ushindi,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Mgunda alisema: “Ni kweli baada ya kufika nilizungumza na wachezaji na kuwaambia kuwa, mafanikio ya mwalimu huanza na wachezaji kwa hiyo wao wawe tayari kwa hilo.
“Maana kama utayari kwao haupo tunaweza kufundisha hadi tukamaliza, hivyo nawashukuru kwa kuonyesha utayari amabapo naamini kazi yetu haitakuwa ngumu kwa kuwa wameonyesha kabisa wako tayari na kuna kitu wataenda kufanya,” alisema Mgunda.