Kumekucha Kenya..Azimio Walaumu Uhuru Kenyatta Kwa ‘Kumuangusha Raila Odinga Uraisi



WANASIASA wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, sasa wameanza kumrushia cheche za lawama Rais Uhuru Kenyatta huku wakidai alisababisha mwaniaji wao wa urais Raila Odinga kuanguka Agosti 9.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamejitokeza wazi kumlaumu Rais ni aliyekuwa Mbunge wa Starehe, Maina Kamanda, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli, wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Caleb Amisi (Saboti) na Seneta wa Narok Ledama Olekina kati ya wengine.

Wanasiasa hao wamemkosoa Rais Kenyatta kwa kutozingatia ushauri na miongozo aliyopewa, huku wengine wakimsifu Rais Mteule William Ruto kwa kuwa na ujuzi wa kipekee wa kisiasa, hali iliyomwezesha kuwashinda kwa urahisi.

Mnamo Ijumaa, Bw Kamanda alidai kuwa hatua ya Rais Kenyatta – anayestaafu Jumanne – kukataa ushauri wa viongozi waliomzidi umri ndani ya Azimio, ilisababisha kuanguka kwa Bw Odinga.


Vilevile, alisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wenye uwazi, kinyume na madai ya viongozi wengi wa Azimio, kuwa ulikumbwa na visa vya udanganyifu na wizi wa kura.

“Tungewezaje kuibiwa kura na washindani wetu ilhali ni sisi tulikuwa tunadhibiti serikali? Hilo ndilo swali la kwanza tunalopaswa kujiuliza. Kwa yeyote aliye Jubilee au Azimio, ni vizuri kukubali kuwa tulishindwa.”

Akaongeza: “Ni vizuri kukubali matokeo ya uchaguzi huo. Ningependa kumwambia Rais wetu [Uhuru], Wakenya walifanya maamuzi yao. Wewe ndiye ulikuwa kiongozi wa nchi hii na mrengo wa Azimio. Wakati kiongozi anapojikwaa, wafuasi wake hujikwaa pia kwenye safari yao. Ulijikwaa, hivyo hatukufanikiwa kukamilisha safari yetu. Tulikosa kupata ushindi kwa sababu ya kuwa na kiongozi ambaye hawezi kushauriwa wala kuambiwa lolote. Huwezi kumwambia [Uhuru] lolote kwani ni vigumu kumwona. Hana kundi la wazee ambao huwa wanamshauri. Hapo ndipo karata zetu kama Azimio ziliharibikia.”


Kwa upande wake, Bw Atwoli alimtaja Dkt Ruto kuwa na mikakati ya kipekee ya kisiasa.

“Sisi tulienda kulala tukijua tumeshinda. Kumbe tulikuwa tukifanya siasa ambayo haina ujuzi. Tulijidanganya kuwa tulikuwa na idadi kubwa ya Wakenya. Badala yake, Ruto alikuwa na mbinu za kisiasa za kipekee ndipo akafaulu kutushinda,” akasema Bw Atwoli.

Bw Owino vile vile alionekana kumwelekeza lawama Rais Kenyatta, akidai alimhadaa kisiasa Bw Odinga.

Sawa na Bw Owino, Bw Amisi alidai Rais Kenyatta alimpotosha Bw Odinga.

Hapo jana Jumamosi, Chama Kitamaduni cha Jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GCA), kilisema kinatambua ushindi wa Dkt Ruto na Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua.

Wadadisi wanasema kujitokeza kwa mabwanyenye hao kutangaza kumuunga mkono Dkt Ruto ni pigo kubwa la kisiasa kwa Rais Kenyatta.

Bw Wilson Rotich, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kisii, hata hivyo, anasema lengo kubwa la Rais Kenyatta lilikuwa kumwachia kiti Bw Odinga ila akazidiwa maarifa na Dkt Ruto.

Marais 20 kushuhudia Ruto akiapishwa
Jaji Mkuu atangaza kanuni mpya kuhusu kusikilizwa kesi za...

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad