Dar es Salaam. ‘Niazime geto lako leo’ ni kauli iliyozoeleka kwa vijana wengi wa kiume ambayo mara nyingi humaanisha kuomba kutumia chumba cha kijana mwenzie kujipumzisha na mpenzi wake.
Ingawa mara nyingi mazoea hayo huwa hayaleti matatizo kwa vijana waliozoeana lakini kwa Tumaini Mabula (32) ‘mchezo’ huo uligeuka shubiri na historia mbaya isiyofutika maishani mwake.
Hadi leo, Tumaini anapambana kuvua maumivu ya kiakili na kisaikolojia yaliyosababishwa na kukaa rumande kwa zaidi ya miaka tisa baada ya rafiki yake kudaiwa kutekeleza mauaji kwenye chumba alichomuachia apumzike na mpenzi wake kilichopo Mwananyamala, Dar es Salaam.
Ilikuwaje?
Februari 17, 2013, rafiki yake, Justin Peter ,waliyefahamiana kwa zaidi ya miaka mitatu alimuomba kutumia chumba chake akiwa mpenzi wake.
“Alikuja kwangu asubuhi saa 2 asubuhi akaomba kuongea na mimi akiwa ameongozana na mpenzi wake. Aliingia ndani na kumuacha yule dada nje akaomba atumie chumba changu, nikamwambia ‘si umpeleke kwa dada yako?’ (alipokuwa akiishi). Akasema haitakuwa heshima,” anasimulia.
Baada ya maongezi mafupi, Tumaini hakusita kutoa chumba chake kwa rafiki yake kwa kuwa halikuwa suala la kumuumiza kichwa.
Aliamua kumpa chumba huku akimwachia maagizo kuwa atakapomaliza kukitumia ampatie ufunguo jirani yake aitwaye Mangi aliyekuwa na biashara ya duka mbele ya nyumba alimoishi au amwachie Janeth aliyekuwa amepanga chumba cha jirani.
Tumaini aliondoka na kwenda katika shughuli zake za kila siku, wakati huo akifanya kazi ya dalali wa vipodozi Kariakoo na jioni ilipofika alirejea nyumbani kwake.
Alipofika nyumba katika nyumba aliyopanga eneo la Mwananyamala, jijini Dar es Salaam alianza kwa kuulizia funguo katika duka la Mangi aliyemjibu kuwa hakuachiwa funguo hizo bali limeachwa deni la soda walizochukuwa wawili hao.
“Nilipiga hatua kuingia ndani nikiamini ameacha funguo kwa Janeth. Nilipomuuliza Janeth alisema hajaachiwa ila aliwaona wageni wake mchana wakienda kununua chakula na wakarudi na ilipofika saa 9 jioni alitoka mwanaume peke yake huku akiwa hana uhakika kama alirudi au la,” alieleza Tumaini.
Majibu hayo yalimfanya ajiulize maswali. Itakuwaje kama bado wako ndani wakati yeye alikuwa amechoka na anahitaji kupumzika? Tumaini aliendelea kujiuliza maswali mengi huku mkononi akiwa amebeba chipsi na ‘CD’ ya filamu aliyokuwa amenunua.
“Wazo likanijia nipige hodi, niligonga mara kadhaa bila majibu, nikaona acha niingie ndani kwa sababu ni kwangu, nilipojaribu kusukuma mlango ulikuwa wazi. Niliingia na kumkuta yule dada amelala chini, nilimuamsha bila mafanikio, nilipoomba msaada kwa majirani hatukufanikiwa mwisho ikabidi tuombe msaada Serikali ya Mtaa,” anaeleza.
Maiti chumbani kwake
Anasema baada ya kutoa taarifa, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa alifika na kumkagua binti huyo na kumwambia ameshapoteza maisha, hivyo alimwamrisha akee chini huku akimweleza kuwa suala hilo liko juu ya uwezo wake.
“Polisi walikuja, wakanifunga pingu, wakampima marehemu na baadaye wakaondoka naye na mimi nikapelekwa polisi,” anasema Tumaini.
Tumaini anasema alipomkuta binti huyo amelala chini hakudhani kama amepoteza maisha kutokana na uelewa wake mdogo.
Alipelekwa Kituo cha Polisi Osterbay na kuhojiwa ambapo aliwajibu askari hakuhusika kwa namna yoyote na mauaji hayo lakini utetezi huo haukumsaidia kwani alishia kuwekwa mahabusu.
Anaeleza kuwa hakuna aliyeamini kirahisi alichokuwa akikiongea na kwamba polisi waliamini kuwa baada ya kukaa naye muda mrefu mahabusu angechoka na kuwaambia ‘ukweli.’
“Nilikaa mahabusu mwezi mmoja na nusu ndiyo nikapelekwa mahakamani, nilisomewa shtaka la mauaji na kurudishwa rumande ambako nilikaa miaka mitatu.
“Kuanzia hapo nilikata tamaa na kukosa kabisa matumaini, awali nilipelekwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni lakini mara ya pili nilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,” anasimulia.
Mshukiwa akamatwa
Baada ya kukaa rumande kwa muda mrefu, hatimaye mwaka 2018 kijana aliyetumia chumba chake alikamatwa katika mpaka wa Tanzania na Burundi akifanya biashara ya kuuza dagaa.
Anasema kimwonekano kijana huyo alikuwa amebadilika kwa kuwa alifuga nywele na ndevu nyingi, hali iliyofanya asitambuliwe kirahisi.
“Alikamatwa na watu wa uhamiaji baada ya kutiliwa shaka. Baada ya upelelezi alitambulika kuwa ni yeye na alipoletwa nilipelekwa kumtambua na kuthibitisha kuwa ni yeye,” anaeleza.
Chanzo cha mauaji
Mabula anaeleza kuwa wakati akihojiwa rafiki yake anasema waligombana na mpenzi wake kupigiwa simu mara nyingi pasi kupokea na baadaye alitumiwa ujumbe mfupi (Sms).
Anasema rafiki yake alimtaka mpenzi wake ampe simu aone ni nani anayepiga simu lakini mpenzi wake aligoma na ndipo walipoanza kugombana na baadaye akaanguka chini.
“Yaani simu hizi tuache kupekuana kabisa maana unaweza kukuta jina lililoandikwa ni tofauti na mhusika”
Tumaini aachiwa
Anasema mwaka 2020 kesi yake ilianza kusikilizwa kwa kasi jambo ambalo lilikuwa likimpa matumaini na kuachiwa huru.
Hatimaye Mei, 2022, aliitwa mahakamani na kusomewa vifungu mbalimbali vya sheria kabla ya kuachiwa huru.
“Nilipoachiwa huru nilinyoosha mkono na kuuliza ‘mheshimiwa umeniachia huru kweli au unanitania, nilimuuliza nje nitaanzaje? Sikutamani kuishi tena uraiani’
“Akaniambia mimi ni kijana nina fursa ya kuanza maisha mapya, kwa kuwa si mlemavu, aliniambia niko huru kwa kuwa mahakamani hakuna utani. Hakimu aliniuliza unakaa wapi? Nikamuambia naishi Mwananyamala. Akaniuliza nauli ni shilingi ngapi? Nikasema Sh300, akaniambia sasa hivi nauli ni Sh500. Akaniambia njoo hapa na kunipa Sh30,000 niondoke,” anasema Tumaini kwa shauku.
Anasema wakati akipitia yote hayo familia yake ilikuwa haijui kinachoendelea jijini Dar es Salaam kwani alipotoka Bariadi, mkoani Simiyu kuja kutafuta maisha Dar es Salaam alikuwa akiwasiliana nao kupitia simu ya jirani.
Alipokuja Dar es Salaam mwaka 2007 alifikia katika Soko la Kariakoo ambapo alikuwa akifanya kazi katika mgahawa wa mama mmoja kwa malipo ya Sh3,000 kwa siku huku akiwa na matumaini siku moja maisha yake yatakuwa mazuri.
“Katika kuangalia nini cha kufanya niliona kuwa madalali wa vipodozi wanapata sana hela, nikajifunza na kuanza kufanya kazi hiyo. Mwaka 2010 ndio nilipanga chumba changu cha kwanza kwa kodi ya Sh15,000 kwa mwezi,” anasema Tumaini.
Tangu kuachiwa, Tumaini alipewa hifadhi katika moja ya fremu za biashara zilizopo Mwenge na baadaye wasamaria wema walimchangia kiasi kidogo cha fedha zilizomwezesha kwenda kupanga chumba kidogo cha kulala tu.
Anaomba msaada wa mtaji wa biashara itakayomwezesha kukidhi mahitaji yake ya kila siku. “Natamani kufungua sehemu ya kuuza matunda lakini pia niwe na kibanda cha kuuza maji na vitu vidogo vidogo,” anasema.
Nitasaidia wafungwa
Licha ya kupitia masahibu hayo, Tumaini hakuwahi kukata tamaa na kumwacha Mungu. Anaahidi kutumia asilimia 30 ya fedha atakayochangiwa kununua vitu vya kuwasaidia watu mbali mbali walioko mahabusu na gerezani.
Kama umeguswa kumsaidia Tumaini unaweza kumpata kwa namba 0693378731 yenye usajili wa jina la Salma Kaswaka