RAIS Mteule William Ruto atajua, ndani ya muda wa saa 36 zijazo, ikiwa ataapishwa Septemba 13 au atarejea debeni huku majaji saba wa Mahakama ya Upeo wakienda faraghani kuamua hatima yake.
Kinara wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga pia anasubiri kujua ikiwa ‘atastaafu’ siasa au atapata fursa nyingine ya kuwania urais iwapo ushindi wa Dkt Ruto utabatilishwa na mahakama hiyo.
Jaji Mkuu Martha Koome na Majaji Philomena Mbete Mwilu, Mohamed Ibrahim, Dkt Smokin Wanjala, Njoki Susanna Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusu kesi ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto Jumatatu.
Katika matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Dkt Ruto alishinda kwa kuzoa kura 7, 176, 142 (asilimia 50.49 ya kura) hali Bw Odinga alipata kura 6, 942, 930 (asilimia 48.85).
Jana Ijumaa, mawakili wa pande zote walihitimisha uwasilishaji wa ripoti zao za mwisho katika jitihada za kushawishi majaji hao saba kukubaliana na misimamo yao katika kesi hiyo.
Wakili Julie Soweto alizua tumbojoto katika mahakama hiyo alipocheza kanda iliyoonyesha jinsi raia wa Venezuela, Jose Camargo alivyovuruga matokeo ndani ya mtandao wa IEBC.
Bi Soweto alisema kuwa jina la raia wa kigeni lilikuwa kwenye Fomu 34A.
“Huyu ndiye mtu aliyekuwa akivuruga matokeo ndani ya mitambo ya IEBC. Hii ilifanyika mnamo Agosti 9 na tuliambiwa kuwa wageni hawa hawakuwepo.
“Tuliambiwa na wakili wa IEBC, Eric Gumbo, wageni hawakuingilia uchaguzi huu. Tuliambiwa kuwa hawakuingilia sava. Lakini katika Fomu hii ya 34A jina la Jose Camargo linaonekana wazi,” Soweto akaambia mahakama hiyo.
Camargo alikuwa mmoja wa raia watatu wa Venezuela waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa JKIA wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Watatu hao walikamatwa na maafisa wa usalama katika uwanja kwa kupatikana na vibandiko ambavyo IEBC ilinuia kutumia katika uchaguzi huo.
Kilichoibua maswali miongoni mwa maafisa hao ni kuwa walikuwa wamebeba vibandiko hivyo katika mikoba yao ya kibinafsi wala hawakuwa wameandamana, wala kupokelewa na afisa yeyote wa IEBC.
Wakili Soweto pia aliuliza ni kwa nini Fomu 34A asilia, ambazo zilikuwa za rangi, zilionekana katika mtandao wa IEBC zikiwa za rangi nyeupe na nyeusi.
“Fomu 34A halisi zilikuwa za rangi na ikiwa picha zao zilitumwa zilivyopigwa mbona zilionekana nyeupe na nyeusi,” akasema.
Wakili huyo huyo pia alionyesha mahakama hiyo jinsi mitambo ya teknolojia ya KIEMs ilikuwa ikituma matokeo ya kuhitilafiana kutoka kaunti za Nyeri na Bungoma.
Lakini wakili wa tume hiyo ya uchaguzi Mahat Somane alipuuzilia mbali madai ya Bi Soweto akishikilia kuwa sava hazikuingiliwa na hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa zilivurugwa.
“Mlikuwa na maajenti katika vituo vya kujumlisha kura katika maeneobunge, ambako kulikuwa na fomu asilia, pia mlikuwa na maajenti katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura. Fomu zilizotumwa zilikuwa halisi,” akasema Somane.
“Vile vile, haiwezeni kuwa mtambo mmoja wa KIEMs unaweza kutuma matokeo tofauti kutoka sehemu tofauti; Mlima Elgon na Nyeri. Kwa hivyo, kauli hii ni ya kubuni na haiwezi kukubalika,” akaeleza.
Kwa upande wake, wakili Tom Ojienda alishikilia kuwa hakuma mgombeaji aliyefaulu kupata asilimia 50 na kura moja ya kura zilizopigwa, ili kuweza kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais.
Profesa Ojienda alikuwa akimwakilisha Seneta Mteule wa Busia Okiya Omtatah ambaye pia aliwasilisha hesabu katika mahakama hiyo kutetea msimamo huo kuwa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga hamna aliyefaulu kupata idadi tosha ya kura kuweza kutawazwa mshindi.
Wakili wa Bw Khelef Khalifa, Willis Otieno pia aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali matokeo yaliyongazwa na Bw Chebukati kwa msingi wa mgawanyiko katika tume hiyo.
Alisema matokeo ya ukaguzi wa kura za urais kutoka maeneo bunge 15 nchini yalionyesha dosari nyingi ambazo zinaweza kuathiri matokeo yaliyotangazwa na IEBC.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu Martha Koome ametoa hakikisho kuwa yeye na wenzake watatoa uamuzi utakaozingatia Katiba na sheria.
Katika hotuba ya mwisho, Jaji aliwaomba mawakili wa pande zote na Wakenya kwa ujumla kuwaombea ili watoe uamuzi wenye “busara kubwa na unaoendeleza demokrasia”.
“Kazi ambayo, tumemaliza leo (jana Ijumaa) ndio ilikuwa ngumu zaidi kuliko ile kazi ambayo tunaelekea kufanya ya kuandaa uamuzi mkubwa utakaokuza misingi ya demokrasia,” akasema Bi Koome.
Kauli yake iliungwa mkono na Naibu wake Jaji Philomena Mwilu.
Polisi wajiandaa kwa sherehe au ghasia Jumatatu