Supastaa Ali Kiba ametangaza kukutwa na virusi vya Corona, hivyo imemlazimu kuahirisha ziara yake ya muziki nchini Marekani ambayo ilikuwa ianze leo Septemba 2.
Kiba ametoa taarifa hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya Kijamii na kuwaomba radhi mashabiki zake ambao walikuwa wakimsubiri kwa hamu nchini Marekani. Hivyo mashabiki wasubiri tarehe mpya itakayotangazwa.
“Kwa mashabiki zangu wote ambao walikuwa wakisubiri kuanza kwa ziara yangu ya muziki “Only One King” mwaka 2022 ambayo ilipangwa kuanza Septemba 2. Ninasikitika kusema kwamba nimegundulika kuwa na virusi vya COVID-19.
“Hivyo basi tumelazimika kuahirisha na kupanga tarehe upya iwezekanavyo. Hakuna chenye umuhimu zaidi kwangu kuliko afya ya bendi yangu, timu yangu na nyie mashabiki zangu. Nina mapenzi makubwa sana kwenu na ninaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.
“Hadi hapo baadae, natumaini kila mmoja wenu atakuwa salama kwa kuchukua tahadhari husika. Inshallah tutaonana hivi karibuni.” - Inasomeka taarifa aliyoitoa Ali Kiba