Maswali Yatawala Mazishi Mtoto Aliyejipiga Risasi



Dar es Salaam. Ibada ya mazishi ya Robert Meier (17) aliyedaiwa kujiua kwa risasi ilifanyika jana nyumbani kwa mzee Matola maeneo ya Kitunda Matembele Dar es Salaam, huku ulinzi mkali ukiimarishwa sambamba na matukio yasiyo ya kawaida na kuwapo kwa maswali kadhaa kutoka kwa waombolezaji.

Robert ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St Mary Goreti iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kujiua Septemba 11 mwaka huu na kuacha ujumbe akitaka mwili wake uchomwe moto.

Hali iliyoonekana siyo ya kawaida ilianza kuonekana nyumbani, kufuatia wanahabari kukatazwa kuchukua taarifa za mazishi na picha.

Aidha baada ya kufika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Augustino –Ukonga, watu waliojitokeza kwenye ibada ya kuaga muda mwingi walionekana kukaa katika vikundi vikundi wakijadiliana na kujiuliza maswali ikiwamo ilikuwaje kijana huyo achukue maamuzi hayo magumu.


Lakini pia baadhi ya waumini walisikika wakihoji sababu ya Paroko kutoka Mwanagati, James Mwinyunge kuja kuongoza ibada kwenye Parokia nyingine, huku wakieleza jambo hilo limewashangaza.

Hata hivyo, baada ya kumaliza mazishi, paroko huyo aliwataka kuacha kujiuliza kwani alitimiza majukumu akiitika wito wa Askofu Mkuu Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi

“Acheni kujiuliza maswali kwa nini nimetoka Parokia moja kuja kuongoza ibada hii. Nimekuja kutekeleza maagizo niliyopewa na Askofu Mkuu,” alisema.

Maswali mengi

Akitoa mahubiri yake Paroko Mwinyunge alisema kifo hicho kimeacha maswali mengi kwa watu wakitaka kujua nini hasa kilichotokea, huku akiwataka wanafamilia na ndugu kuacha kujiuliza na kwamba wamuombee.

“Watu wanajiuliza maswali mengi na wanajikuta bado wako gizani wakiwa hawajui sababu hasa iliyosababisha kifo cha Robert lakini niwasihi wazazi, wanafamilia na ndugu jamaa na marafiki kuacha kujiuliza maswali na kikubwa muombee safari njema,” alisema.

Akitoa nasaha, mwalimu na mwakilishi wa Shule ya St Mary Goreti, Ringia Ulomi, alimuelezea kijana huyo kwamba alikuwa mpole na aliyekuwa na bidii ya kusoma, huku akieleza ndoto yake ilikuwa kuja kuwa mwanasheria.

Akisoma wasifu wa Robert mmoja wa wanafamilia wa Mzee Matola alisema Robert alizaliwa mwaka 2005 mkoani Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad