Moshi/Dodoma. Mawakala 21 wa pembejeo ambao ni kati ya mawakala zaidi ya 300 nchini waliosambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima mwaka 2015/2016 na kuidai Serikali kwa miaka saba sasa, wameelezwa kufariki dunia wakisotea malipo hayo.
Ukiacha waliofariki, miongoni mwa mawakala hao, wapo waliofilisiwa na taasisi za fedha zikiwamo benki kutokana na kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati na wengine wakipata ugonjwa wa shinikizo la damu.
Malipo ya mawakala hao ambayo ni zaidi ya Sh38 bilioni, yalisitishwa na Serikali mwaka 2016, ili kupisha uchunguzi baada ya kubainika kuwapo udanganyifu uliofanywa na baadhi ya mawakala.
Mawakala hao wachache walidaiwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Wizara ya Kilimo kufanya udanganyifu na kuwasilisha Wizara ya Fedha madai ya zaidi ya Sh70 bilioni, hali iliyoisukuma Serikali kusitisha malipo, ili kuruhusu uchunguzi.
Hata hivyo, suala hilo limechukua muda mrefu kufikia mwisho, licha ya mawakala kutoa ushirikiano kwa taasisi za uchunguzi ikiwamo Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku baadhi wakifariki dunia kabla hawapata haki yao.
Miezi sita iliyopita, Mbunge wa Kalenga (CCM), Jackson Kiswaga aliuliza swali bungeni kuhusiana na malipo ya mawakala hao ambapo Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema uhakiki wa malipo hayo ulikuwa hatua za mwisho.
Mwananchi lilimtafuta Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe juzi na kumuuliza ni lini mawakala hao waliosota kwa miaka saba sasa watalipwa malipo kwa waliohakikiwa, alisema ni vigumu kueleza ni lini watalipwa.
Waziri Bashe ambaye pia ni mbunge wa Nzega mjini, alisema ni vigumu kujua kwa sababu wasambazaji hao walipeleka madai ya zaidi ya Sh40 bilioni, lakini yalipochambuliwa yaligundulika kuwa ni zaidi Sh20 bilioni.
“Madai hayo yalienda ofisi ya CAG bado hayajarudi. Siwezi kusema sasa watalipwa lini kwa sababu yakimalizwa katika ofisi ya CAG yatakwenda Wizara ya Fedha na Mipango.
“Wengi wana malalamiko kuhusiana na kuchelewa kulipwa kwa madai yao, lakini ni vyema kujiridhisha kabla ya kulipa,” alisema.
Mawakala wafunguka
Baada ya kauli ya waziri Bashe, mwenyekiti wa Ushirika wa mawakala hao, Tanzania Agro Dealers Cooperative Society (TADCOS), Gerold Mlenge, aliiomba Serikali kuwatizama kwa jicho la huruma.
“Sisi kwa sasa hatuna doubt (mashaka). Kikubwa kwanza yafanyike hayo malipo hata kama yatakuwa ya mazingira yoyote kwa sababu kama ni suala la kusubiri tumeshasubiri katika kipindi kirefu sana”alisema Mlenge alipozungumza na Mwananchi juzi.Alisema wanazungumzia vitu ambavyo vipo isipokuwa wanashindania kiwango.
“Wao wafanye utekelezaji na ambaye ataona ameonewa katika malipo atachukua hatua za kufanya. Tunataka hili lifanyike kwa wakati kwa sababu sasa tunashindwa kumsaidia mama kwenye hili jambo lake la mbolea za ruzuku,” alisema na kuongeza:
“Agro Dealers wengi hatujaingia kusambaza mbolea ya ruzuku ingawa tumechaguliwa, tunashindwa kwa sababu hatuna mitaji.
“Duka nilifunga 2018 baada ya kuona nimefilisika, lakini benki wameuza nyumba zangu mbili nilizokopea na nikauza malori yangu mawili na basi moja, ili nimalize mkopo wa benki.”alieleza.
Alisema hayo ni kwake, lakini kuna wengine 21 wameshafariki dunia wakiendelea kusotea madai yao.