Mawakili wa timu ya wanasheria wanaomtetea Raila Odinga, wakiongozwa na Julie Soweto, wamedai kura 4,463 zilitolewa kutoka kwa mteja wake na kuongezwa kwa Rais mteule William Ruto katika Kaunti za Bomet, Kiambu, Kakamega, Nairobi na Baringo.
Bi Soweto ameiambia mahakama kuu nchini Kenya leo Jumatano kwamba kulikuwa na tofauti katika fomu 41 za 34A kutoka Bomet, Kiambu na Kakamega zilizopewa maajenti na zile zilizopo kwenye tovuti ya IEBC, ambazo ziliwasilishwa katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura cha Bomas.
"IEBC ilinunua seti mbili za fomu 34A licha ya kutakiwa kununua kijitabu kimoja pekee ambacho kingetumiwa katika vituo vya kupigia kura huku 2/2 kikihifadhiwa kwenye bahasha isiyoweza kuguswa. Hati ya kiapo ya Celestine Anyango inaonyesha ubaya wa kimakusudi katika matumizi ya fomu.
Fomu ambazo mawakala wanazo na fomu kwenye tovuti ni sawa katika vipengele vyote (namba za mfululizo, mihuri, sahihi). Hata hivyo, takwimu katika fomu zimebadilishwa na ni tofauti," alisema.
Awali, wakili Mkuu James Orengo, ambaye pia katika timu ya wanasheria wa Bw Odinga, alidai kuwa IEBC haina utendakazi na haiwezi kufanya uchaguzi. Pia alidai kuwa fomu hizo zilibadilishwa.