Mbaroni kwa kuwalewesha wanawake na kuwaibia
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Fortunatus Musilimu, alikiri jana kukamatwa kwa watu hao kwa nyakati tofauti kwa madai ya kujihushisha na vitendo hivyo kwenye mikoa mbalimbali nchini ikiwamo Morogoro, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam.
Baada ya kuwafanyia hivyo, watu hao huwaibia fedha simu na mali zingine na baadhi yao kuwaingilia kimwili bila ridhaa yao.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Paulo Shayo (48) mkazi wa Kihonda Maduka 10, Manispaa ya Morogoro na Dixon Mwashambo (33) maarufu kama Tajiri Maswe au Papaa, mkazi wa Buza Tanesco, Dar es Salaam ambaye hujihusisha na shughuli za udalali.
Kamanda Musilimu alisema watu hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitumia unadhifu wao, magari ya kifahari na ya gharama kubwa, kuwarubuni kimapenzi na kujenga uhusiano na wanawake hasa wenye kipato kikubwa na kuwapeleka kwenye hoteli kubwa, wakiagiza vyakula na vinywaji vya gharama kubwa.
Pia alisema watuhumiwa hao huwawekea wanawake hao dawa za kulevya zinazosadikiwa kuwa ni vidonge vinavyoyeyuka kirahisi kwenye supu au vinywaji na hatimaye wanapoanza kuvurugukiwa hutoa namba za siri za benki, simu na taarifa zingine nyeti kisha kuwaibia.
Kuhusu Shayo, alisema amekuwa akitumia mbinu ya kuwapeleka wanawake kwenye hoteli za kifahari na kuwapa vitambaa vya kufutia jasho (leso) viinavyosadikiwa kuwa na dawa za kulevya, hivyo muda mfupi baada ya kuvitumia kupoteza fahamu kisha kutekeleza uhalifu.
Musilimu alibainisha moja ya matukio ya hivi karibuni alilofanya ni kwenye hoteli ya Cate iliyoko barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam mjini Morogoro, eneo la Kingoluwira.
Alisema mtuhumiwa huyo alimwibia binti mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa Dakawa na mdogo wake mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Kihonda Bima, fedha tasilimu Sh. milioni 1.6 na simu mbili aina ya Vivo na iPhone 7.
Papa au Tajiri Maswe, Musilimu alisema amekuwa akitumia mbinu ya kuvaa kwa unadhifu na kujifanya ni mtumishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) makao makuu, Dodoma.
Katika kutekeleza uhalifu wake, alisema mtu huyo akikutana na mwanamke ambaye ameshamrubuni hununua supu au mvinyo mwekundu (red wine) na kuweka dawa za kupoteza kumbukumbu kisha kumfanya atoe namba za siri za kampuni za simu na akauti za benki na kuwa rahisi kumwibia.
"Tukio la karibuni, mtuhumiwa Mwashambo alilifanya baada ya kuingia Morogoro majira ya saa 12:00 jioni akitokea Dar es Salaam. Alimwibia binti mwenye umri wa miaka 27, mkazi wa Mlandizi mkoani Pwani kwa kuchukua Sh. milioni 7.45, simu aina ya iphone 8+ na saa aina ya Rado,” alisema Musilimu.
Alisema mtuhumiwa alimrubuni mwanamke huyo baada ya kumwomba msaada wa usafiri baada ya basi kuharibika njiani eneo la Dumila, badala yake akampeleka binti huyo hadi kwenye kwenye nyumba ya kulala wageni ya SAS iliyoko mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa Kamanda Musilimu, mtuhumiwa huyo anadaiwa amekuwa akibaka na kuwalawiti watu anaofanikiwa kuwarubuni na amekuwa alijihusisha na matukio hayo ya kiuhalifu katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando, alizungumzia Kamati ya Ulinzi na Usalama ilivyopata taarifa za matukio ya kiuhalifu kwa wanawake yanayofanywa na mtuhumiwa Shayo na kuingilia kati kutafuta taarifa zake hadi walipomtia mbaroni na kuwakabidhi polisi.
"Shayo licha ya kuwatapeli mabinti hao mtu na mdogo wake, aliwatelekeza hoteli ya Cate na kuwaachia deni la zaidi ya Sh. 700,000 na kufanya mabinti hao kupelekwa polisi.
“Awali, alichukua vyumba viwili katika hoteli hiyo na kukaa na hawa mabinti kwa siku tatu mfululizo akitoa ofa kwa watu mbalimbali na kununua vinywaji vya gharama. Akiwa hapo aliwawekea dawa za kulevya na kuwalevya kisha kuchukua simu zao na kujitumia fedha zaidi ya milioni moja kwenye akaunti yake," alisema Msando.
Kwa mujibu wa Msando, baada ya uhalifu huo, mtuhumiwa alitoroka hotelini na kuwatelekeza mabinti hao huku kukiwa na deni la bili ya zaidi ya Sh. 700,000 hatua iliyosababisha mabinti wakamatwe na kupelekwa kituo cha Polisi Kingoluwira lakini baadaye akaagiza wafikishwe Kituo Kikuu cha Polisi.