Mfahamu Rais wa Afrika Mwenye Umri Mkubwa zaidi Duniani

 


Rais wa Cameroon, Paul Biya sasa ndiye mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II wa Uingereza siku ya Alhamisi.


Buckingham Palace, Septemba 8, 2022 ilitangaza kwamba Malkia Elizabeth II alifariki kwa amani huko Balmoral – Scotland akiwa na umri wa miaka 96, ambapo Rais huyo wa Cameroon aka ‘tweet’ ujumbe ufuatao.


“Kifo cha Elizabeth II kimeleta simanzi na athiri kwa nchi wananchama wa Jumuiya ya Madola kutokana na ukweli kuwa alikuwa na uongozi wa kipekee na aliiwakilisha vyema nembo ya historia yake.”

Mtawala huyo mwenye umri wa miaka 89, amekuwa kwenye usukani wa uchumi mkubwa zaidi wa Afrika ya kati kwa miaka 40, na iwapo miaka yake saba ya awali kama Waziri Mkuu itaongezwa katika utawala wake wa miongo minne, basi Biya angekuwa kiongozi wa muda mrefu zaidi asiyekuwa wa kifalme aliyetawala Duniani.


Biya, anafuatwa kwa umri na Jenerali wa zamani wa kijeshi, Michel Naim Aoun mwenye umri wa miaka 88 ambaye amehudumu kama Rais wa Lebanon tangu Oktoba 2016.


Chini ya utawala wa Paul Biya, Cameroon ilinusurika kudorora kwa uchumi katikati ya miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, na kusababisha siasa za uhamaji kutoka chama kimoja hadi Serikali ya vyama vingi.


Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea, Rais aliyekaa madarakani kwa miaka 39 hadi kufikia mwaka 2018, akitawala toka mwaka 1979. Picha na AP

The Lion Man, kama kiongozi wa octogenarian anatajwa kwa upendo na wanachama wa chama tawala cha Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM), na wafuasi wake walikubali siasa za vyama vingi miaka ya 90, ingawa ameendelea kuwa mshindi wa uchaguzi wa mfululizo, huku vyama vya upinzani vikidai kuibiwa kura kama ilivyo ada ya ala hizi za malalamiko yasiyo na matokeo chanya katika Bara la Afrika.


Cameroon, imekuwa na wakuu wa nchi wawili pekee tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wafaransa mwaka 1960, Rais wa kwanza akiwa ni Ahmadou Ahidjo ambaye baadaye alimuachia utawala Waziri wake Mkuu, Paul Biya ambaye aliapishwa kwa mara ya kwanza kama Rais wa nchi hiyo, mwaka 1982.


Cameroon ina idadi kubwa ya vijana, na zaidi ya asilimia 60 ya watu chini ya umri wa miaka 25 na Biya akaibua matumaini aliposhika usukani, lakini hata hivyo muda wake wa uongozi umekumbwa na utata baaba ya kile kilichotarajiwa na watu wengi kuwa na matokeo hasi.


Denis Sassou Ngueso, hadi kufikia mwaka 2018, alikuwa ameiongoza Jamhuri ya Congo ya Brazzaville kwa miaka 34 tangu aliposhika madaraka ya kuliongoza Taifa hilo mwaka 1984. Picha na Glamtush.

Hali hii, ilimfanya Paul Biya kukosolewa vikali kwa utawala wake wa kimabavu na ufisadi uliokithiri katika nchi hiyo ambayo mwananchi wa kawaida anaishi chini ya dola 2 kwa siku kitu ambacho kikazalisha manung’uniko na uasi kwa baadhi ya maeneo na wengine kujitenga na kutoa pande mbili zinazopingana za wanaozungumza lugha ya Kifaransa na Kiingereza.


Hali hii, ilifanya Mataifa mengi kuelekeza macho yote katika jiji la Yaounde na baadaye ripoti ya Shirika la Transparency International, likaitaja Cameroon kuwa ‘nchi fisadi zaidi duniani’ na hapo ndipo ilipo orodheshwa kama Taifa la juu zaidi lenye matukio ya kifisadi hiyo ilikuwa mwaka 1998 na 1999.


Paul Biya, pia amekuwa na sifa mbaya kama rais ambaye anaweza iongoza Cameroon akiwa nje ya nchi, akitumia pesa nyingi za walipa kodi katika hoteli za kifahari nchini Uswizi, na inaelezewa kuwa huko anamiliki jengo la kifahari na hujipa likizo ya kudumu akitaka.


Idris Deby wa Chad, ambaye aliliongoza Taifa hilo kwa miaka 24 hadi kufikia mwaka 2018, alishika madaraka ya kuliongoza Taifa hilo mapema mwaka 1994. Picha na CFR.

Inasadikika kuwa, mara kwa mara Biya huelekea katika nchi ya Alpine kwa mapumziko katika Hoteli ya Intercontinental iliyopo huko jijini Geneva nchini Uswisi kwa ajili ya kula raha za Dunia na kumwagilia moyo, huku akiliacha Taifa hilo katika majonzi ya makali ya maisha yanayozua mijadala kuhusu kesho ya Taifa hilo.


Hii, ilifanua uchunguzi wa 2018 wa Mradi wa Kuripoti Uhalifu na Ufisadi uliopangwa (OCCRP), kukadiria kuwa Biya alitumia takriban siku 60 kwenye ziara za kibinafsi nje ya nchi, na pia inaarifiwa alitumia theluthi moja ya mwaka akiwa nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka 2006 na 2009.


Hata hivyo, wafuasi wa Biya waliielezea ripoti hiyo kama “propaganda”, ndipo ripoti nyingine ikatolewa ikisema kiongozi huyo alitumia dola milioni 182 kwa safari zake za kibinafsi tangu awe rais na kwamba pia alitumia dola 40,000 kwa siku kwa ajili ya malazi ya hoteli ya yeye na wasaidizi wake.


Sarakasi zikaendelea, kwa Paul Biya bila kuwa na sifa za kugombea akachaguliwa tena kwa muhula wa sita mwaka 2011, kufutia Bunge linaloongozwa na chama tawala kupiga kura ya kurekebisha katiba, kuondoa ukomo wa mihula ya urais na kwa kuichezea katiba, Biya akapata nguvu ya kusalia madarakani kwa muda usiojulikana.


Kwa bara la Afrika, Viongozi wanaotajwa kuwa madarakani kwa muda mrefu zaidi hadi kufikia mwaka 2018 ukimuacha Rais Paul Biya ambaye hadi mwaka huu wa 2022 anafikisha miaka 40 madarakani ni pamoja na Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea (39), Denis Sassou Ngueso wa Jamhuri ya Congo (34), Idris Deby wa Chad (28) na Yoweri Kaguta Museven wa Uganda ambaye mpaka mwaka huu wa 2022 anafikisha miaka 36 madarakani.


Bila shaka, huenda una mawazo na maswali mengi kichwani mwako juu ya simulizi hii, lakini acha nikukumbushe kitu, “Kila kizazi huwa kinajiona kina akili nyingi zaidi kuliko kizazi kilichotangulia na pia hujiona chenye hekima sana kuliko kizazi kinachokuja baadaye.” Hivyo basi acha usiwaze wala kukihofia kivuli, tambua kwamba palipo na kivuli kuna mwanga, pambana ili mwanga ukuangazie.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad