Mimi siumii na tozo naumia na matatizo ya wananchi



Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema kwa upande wake anaumizwa zaidi na shida za wananchi kuliko baadhi ya watu wanavyodai kuumizwa kwa kukatwa Tozo

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wakuu wa mikoa ya Nyanda za Juu kusini - Iringa, Rukwa, Mbeya na Katavi uliofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom) Homera amesema wananchi wa Mbeya hawalalamiki kuhusu tozo na badala yake wanaendelea kuchangia maendeleo yao wenyewe

"Watanzania waliopo Mbeya hili suala la malalamiko ya tozo huku hakuna, sisi tunahangaikia kuhakikisha huduma za afya zinaimarika kwa kuchangia sisi wenyewe watanzania" amesema RC Homera

"Mimi siumii na tozo naumia zaidi na matatizo ya wananchi wangu wa mkoa wa Mbeya, kama tumejenga kituo cha afya na leo wameacha kutembea umbali mrefu kufuata huduma kwa sababu ya tozo, kwanini nisiwe sehemu ya kufurahia"

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya RC Homera ameeleza baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa mkoani humo
"Rais Samia amefanya maajabu mkoa wa Mbeya, amejenga vituo vya tiba zaidi ya 365, ikijumuisha hospitali 21, vituo vya afya 36 na zahanati 308"


"Watanzania waliopo Mbeya wananufaika na mfuko wa asilimia 10, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na sasa tumebadilisha mfumo badala ya kuwapa watu pesa wakagawane sasa tunajenga viwanda"

Katika mkutano huo mkuu wa mkoa wa Iringa Halima Dendego amesema mkoa huo umepiga hatua kubwa kiuchumi ikiwemo kupanda kwa pato la mwananchi mmoja mmoja kwa mwaka

"Mkoa wa Iringa umepiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi, lakini umeweza kuongeza pato la mkoa kwa kiwango kikubwa, lakini pato la mwananchi wa Iringa limeongezeka kutoka shilingi milioni 3.5 kwa mwaka mpaka milioni 4.028 na kufanya Iringa kuwa mkoa wa pili kwa wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka"


"Mkoa wetu una vijiji 360 katika vijiji hivyo ni vijiji 33 tu havina umeme na hivi navyozungumza tayari kuna mkandarasi yupo kazini na tukifika Desemba vijiji vyote vitakuwa na umeme" amesema RC Dendego

Naye mkuu wa mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amewakaribisha watanzania na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza huku akiwahakikishia usalama wao 

"Rukwa ni mkoa salama sana, tangu nimekuja sijawahi kulala nje, sijaumwa tumbo, sijavimva kichwa na sijabadilika mahala, kwahiyo ninawakaribisha wote wanaokuja kuwekeza, wajue ni sehemu salama na hakuna mambo ya jadi" ameeleza Queen Sendiga, Mkuu wa mkoa wa Rukwa

Awali akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema miradi mbalimbali ya maeneleo inaendelea kukamilika mkoani humo ikiwemo bandari ya Karema ambayo itachochea ukuaji wa uchumi


"Katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita ujenzi wa bandari ya Karema ambao umegharimu takribani shilingi bilioni 47.9 sasa bandari imekamilika na imeanza kutumika tangia tarehe moja Septemba"

Kuhusu afya mkoani Katavi RC Mwanamvua amesema fedha za tozo zimesaidia kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
"Tuna vituo vya afya sita ambavyo vimepata takribani bilioni 3 kutokana na tozo, na vituo hivyo kuna ambavyo vimekamilika, na nasema kwa mfano fedha hizi zingekuwa hazipo tungepata bajeti ya serikali ila miaka kadhaa mbele"
 


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad