Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Ernest Khisombi amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za kujipatia mkopo wa gari binafsi wenye thamani ya Shilingi 196.57 milioni.
Mkurugenzi huyo amefikishwa mbele ya Baraza hilo la maadili Septemba 12, 2022 kwa kujikopesha kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Akisoma mashtaka mbele ya Baraza la Maadili, Wakili wa Serikali Hassan Mayunga ameliambia Baraza kuwa, mtuhumiwa anashtakiwa kwa makosa mawili ambayo ni kukopa fedha za mfuko kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 117 bila kufuata utaratibu.
Katika lalamiko hilo Na. 5 la mwaka 2022, kosa la pili ni kulipiwa kodi zaidi ya shilingi milioni 78 bila kufuata utaratibu wa Sera ya Mikopo ya PSSSF.
Kwa mujibu wa Mayunga, kitendo hicho kinamfanya Khisombi ambaye ni Kiongozi wa Umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushidwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na (b) na hivyo kukiuka maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha Sharia ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo, Khisombi amekana tuhuma hizo na kulieleza Baraza la Maadili kuwa, “fedha hizi ni haki yangu kama Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi kwa mujibu wa Sera ya Mikopo ya Mfuko.”
Shahidi wa mlalamikaji Gideon Mafwiri ameliambia Baraza kuwa kiongozi huyo alijipatia mkopo kinyume na utaratibu uliowekwa na mfuko wa mikopo wa PSSF.
“Mfuko wa mikopo umeweka utaratibu wa ni viongozi wapi wanastahili kulipiwa kodi na mfuko nan i gali la namna gani litalipiwa kodi na mfuko kwa mujibu wa taratibu,” alisema Mafwiri.
Kwa mujibu wa maelezo ya shahidi, utaratibu wa Mfuko ni kuwa maombi ya mkopo yanaidhinishwa na Kamati ya Mkopo ya Mfuko, mkopaji kulipia asilimia 5 ya mkopo kabla hajapatiwa mkopo pamoja na kulipiwa kodi gari jipya la kiongozi kwa asilimia 100.
“Sera ya mikopo ukurasa wa 10 inasema mkopo huo utalipiwa asilimia 5 kabla mkopaji hajapatiwa. Lakini Utaratibu huu haukufuatwa,” ameongeza.
Mafwiri ameeleza kuwa wakati mfuko unalipia kodi ya gari la Khisombi, gari hilo halikuwa jipya kama Sera ya Mfuko huo inavyoelekeza. Ushahidi wa shauri hilo Na. 5 la mwaka 2022 umekamilika na kufungwa kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Baraza la Maadili lililoanza vikao vyake vya uchunguzi Septemba 6, 2022, limekwisha sikiliza malalamiko mengine kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongizi wa Umma dhidi ya Godfrey Chibulunje aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu katika Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Hoseah Kashimba, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Beatrice Lupi, Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Baraza hili linaloongozwa na jaji Ibrahimu Mipawa na wajumbe Peter Ilomo na Suzan Mlawi linafanya uchunguzi wa wazi kwa mujibu wa Kifungu cha 25 (5) na 29 (6) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Sura 398).